Breaking

Monday, 25 March 2024

DK. NCHIMBI ATETA NA SHEIN NA SALMIN ‘KOMANDOO’

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi, amesema ushauri na maelekezo ya Viongozi Wastaafu wa Chama na Serikali, pamoja na Wazee wa CCM kuhusu umuhimu wa kuendelea kukiimarisha Chama, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwatumikia watu vizuri, yatafanyiwa kazi kwa uzito unaostahili.

Katibu Mkuu Balozi Dk. Nchimbi amesema hayo Jumapili, Machi 24, 2024, wakati wa mazungumzo na viongozi wastaafu wa Chama na Serikali, wakiwemo Marais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Wenyeviti wa Baraza la Mapinduzi (wastaafu), Dk. Salmin Amour Juma na Dk. Ali Mohamed Shein, nyakati tofauti katika makazi yao, pamoja na Wazee wa CCM kwenye mikutano yao ya mabaraza, Pemba na Zanzibar.

“Asanteni. Waambie pia nawasalimia. Simamieni Chama…chama kijengwe, kisimamiwe kupata ushindi mzuri,” amesema Dk. Salmin Amour, baada ya kufikishiwa salaam za Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussen Ali Mwinyi, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.

Kwa upande wa Dk. Shein, amesisitiza umuhimu wa CCM kuendelea kusimamia misingi ya kuanzishwa kwake.

“CCM ni chama makini sana. Kina misingi na taratibu zake. Na jambo zuri ni kwamba Katibu Mkuu ndiye msimamizi. Nakujua, tumekuwa wote Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa muda mrefu. Sina shaka nawe kuyasimamia haya. Tukipindisha taratibu tutaanza kwenda kombo. Jengine ni suala la usiri wa vikao, lazima vikao viwe na siri,” amesema Dk. Shein.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages