Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Magomeni imeendelea na zoezi la kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi wa mitaa ya Mpiji, Chimwaga, Madukani na Namnani Kata ya Sinza D baada ya kukamilika kwa maboresho katika mtambo wa Ruvu Chini hivi karibuni.
Akizungumza wakati wa ufuatiliaji upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo hayo, Meneja wa Mkoa wa Kihuduma DAWASA Magomeni, Bi. Julieth John ameeleza kuwa upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Kata ya Sinza D unaendelea kuimarika siku hadi siku na hivyo kuleta matumaini kwa wakazi wa eneo hilo.
"Huduma ya maji kwenye mitaa ya Madukani, Mpiji na Namnani katika Kata ya Sinza D imeanza kurejea mara baada ya kukamilika kwa maboresho ya miundombinu ya mifumo ya usambazaji maji kwenye Mtambo wa Ruvu Chini," ameeleza Meneja Julieth.
Bi. Julieth amewasisitiza wananchi kuendelea kuwa watulivu kwani Mamlaka ipo kazini usiku na mchana kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora na endelevu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sinza D, Ndugu Muumini Herezi ameishukuru Mamlaka kwa jinsi inavyozidi kutatua changamoto za wananchi katika upatikanaji wa huduma ya maji.
"Nachukua fursa hii kuwashukuru sana DAWASA kwa jitihada wanazozifanya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji pamoja na kushughulikia kero zao hasa katika suala la maji," ameeleza Ndugu Herezi.
Mkazi wa Mtaa wa Mpiji Kata ya Sinza D, Bi. Brunide Mbaga ameishukuru Mamlaka kwa kutatua changamoto ya mgao wa maji na kuiomba Mamlaka iwafikie wateja wengi zaidi kwani huduma ya maji ni muhimu kwa wananchi wote.
"DAWASA ijitahidi kuongeza nguvu katika kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wote, maana huduma ya maji ni muhimu sana," ameeleza Ndugu Mbaga.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990