Imeandaliwa na: James Ndege – Ifakara.
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Kanda ya Kati Dodoma inafanya kampeni ya wiki moja ya kutoa elimu right usalama, ubora na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika shule za sekondari na makundi mbalimbali ya kijamii katika halmashauri za Ifakara na Mlimba kuanzia tarehe 29 Januari hadi 02 Februari, 2024.
Lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha kwamba jamii yote ya watanzania mijini na vijijini inakuwa na uelewa mkubwa wa matumizi sahihi ya bidhaa hizo zinazodhibitiwa na TMDA ili kuepusha madhara ya kiafya yanayoweza kutokea kutokana na matumizi yasiyo sahihi.
“Matumizi yasiyo sahihi ya dawa ikiwa ni pamoja na kutumia dozi isiyokamilifu (nusu dozi) au dozi kubwa tofauti na ilivyoshauriwa na wataalam wa afya huweza kusababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na viungo vya ini na figo kushindwa kufanya kazi”.
“Madhara mengine ni kusababisha usugu wa vimelea vya maradhi dhidi ya dawa kama zile za malaria na antibiotiksi (vijiuasumu) na nyinginezo. Hivyo mgonjwa anapaswa kutumia dawa baada ya kupata ushauri wa wataalam waliopo katika kituo cha kutolea huduma za afya atakachokwenda mgonjwa”, alieleza Bi. Serafina Omolo ambaye ni Mkaguzi Mwandamizi wa TMDA Kanda ya Kati.
Katika hatua nyingine, ilielezwa kwamba katika kampeni hiyo TMDA imeweza kufungua klabu za TMDA zipatazo 11 katika shule za sekondari za Mang’ula, Kisawasawa, Kibaoni, Kilombero, Bravo, Kiyongwile, Mlabani, Mchombe, Kihule, Kiburubutu na Nakaguru za halmashauri hizo mbili ili kuwa na elimu endelevu. Aidha, viongozi mbalimbali wa kata wapatao 16, wananchi 301 walipata elimu hiyo mubashara.
“Kwa zaidi ya miaka minne sasa, TMDA hurusha kipindi cha runinga kinachojulikana kama TMDA na Jamii sanjari na kutumia vituo vya redio vyenye wigo mkubwa, redio na mitandao kijamii katika kufikisha elimu kwa umma hivyo endeleeni kufuatilia ili mpate elimu zaidi kwa nia ya kulinda afya zenu”, alisema Bi. Serafina.
Wazazi wa wananfunzi wa shule ya Sekondari Kinyongwile katika Hamashauri ya Mji Ifakara wakifuatilia mada ya TMDA kutoka kwa mwasilishaji (hayupo pichani)
Bw. James Ndege, Afisa Mwandamizi wa TMDA akisisitiza jambo kwa wanafunzi ya Shule ya Sekondari Kiburubutu wilayani Mlimba.
Picha ya pamoja baina ya Maafisa wa TMDA, Watendaji wa Kata ya Mwaya na waalimu wa Shule ya Sekondari Mang’ula – Ifakara baada ya kujumuika na wanafunzi kupata elimu ya matumizi sahihi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi