Na Mwandishi Wetu, Arusha
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kaskazini limefanya ukaguzi na kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa bidhaa za kuokwa (mikate, mandazi, nk) mkoani Arusha ili kuhakikiza wanazalisha bidhaa hizo kwa kufuata taratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki mara baada ya kumalizika ukaguzi huo na utoaji elimu mkoani hapa, Meneja wa TBS Kanda ya Kaskazini inayojumuisha Mikoa ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Manyara, Joseph Mwaipaja, alisema ukaguzi na elimu hiyo ilitolewa kwa wananchi na wajasiriamali wanaozalisha bidhaa hizo ili bidhaa zao zinapoingia sokoni ziwe zinakidhi matakwa ya viwango.
"Tulianza kwa kutoa elimu kwa kuwaelezea njia sahihi za kuzalisha bidhaa za kuokwa ili wajue kwamba sio halali kwao kuendeleza kuuza bidhaa ambazo hazijakidhi matakwa ya ubora," alisema Mwaipaja.
Alifafanua kwamba ukaguzi huo unaenda mbali zaidi hadi kwenye maduka wanakouza bidhaa hizo kwa sababu kwa mamlaka waliyopewa na sheria, TBS inasajili maghala, maduka na supermakert, hivyo wahusika wanatakiwa kuruhusu kuingia bidhaa ambazo zimethibitishwa na shirika hilo.
Kwa mujibu wa Mwaipaja endapo watabaini bidhaa za kuokwa ambazo hazijakidhi matakwa ubora wataziondoa na kuziharibu kwa gharama za hao wafanyabiashara wanaoendelea kuzalisha bidhaa ambazo hazina ubora.
Aliwahimiza wazalishaji hao kuthibitisha ubora wa bidhaa zao, kwani kufanya hivyo kuna faida nyingi.
Alitaja baadhi ya faida hizo, akisema kwanza Arusha ni mkoa wa wa kitalii hivyo wanataka hata bidhaa ambazo watalii na Watanzania kwa ujumla wanazitumia ziwe ni zile zilizothibitishwa ubora na TBS.
"Kwa hiyo wakithibitisha bidhaa zao wataweza kuuza kwenye supermakert, pili kuwafanya wanunuzi kujiamini kwamba bidhaa husika ni salama kwa afya ya mlaji baada ya kuwa zimethibitishwa na shirika letu," alisema Mwaipaja na kuongeza;
"Kwa kufanya hivyo wanaongeza wigo wa bidhaa zao kwa sababu zinakuwa zinatambulika."
Alitaja faida nyingine za kuuza bidhaa zenye ubora kuwa ni pamoja na kuwa na biashara ambazo ni endelevu, kwani taasisi za kifedha zinamuelewa mfanyabiashara mwenye biashara endelevu, hivyo inakuwa ni rahisi kwake kwenda kuomba mkopo ili kuweza kutanua biashara yake.
Kwa mujibu wa Mwaipaja ukaguzi wa bidhaa za kuokwa na utoaji kwa mikoa ya kanda ya kaskazini litakuwa endelevu na kwa miezi miwili iliyopita wamekuwa wakifanya ukaguzi wa bidhaa ambazo hazina ubora.
"Lakini kwa sasa hivi tumeanza na mikate kwa sababu kuna watu wanaona ni haki kwao kuuza bidhaa ambazo hazina nembo ya TBS.
Kwa hiyo kwa mikoa yote ya kanda ya kaskazini wajue kwamba TBS tupo kazini tutaenda kila mkoa na tukibaini hizo bidhaa tutaziharibu," alisema.
Alitoa wito kwa wazalishaji kufika TBS kuanza mchakato wa uthibitishaji ubora wa bidhaa.