Na Zainab Ally -Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mh.Dkt. Hussen Mwinyi amefurahishwa na uhamasishaji wa utalii na fursa za uwekezaji unaofanywa na TANAPA, wanaoshiriki maonesho ya The Z - Summit yaliyofunguliwa katika ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar.
Katika maonesho hayo yaliyozinduliwa leo tarehe 21.02.2024 na Rais huyo, TANAPA wameungana na wadau mbalimbali wa utalii kutoka mataifa tofauti duniani ili kuuza na kununua bidhaa zinazotokana na mazao ya utalii huku TANAPA ikinadi na kuhamasisha fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Hifadhi za Taifa.
Akiwa katika banda la Wizara ya Maliasili na Utalii Rais Mhe. Dkt. Mwinyi alielezwa vivutio na fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya Hifadhi za Taifa 21 zinazosimamiwa na TANAPA, na kuridhishwa na Shirika hilo linavyojitoa kulinda rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Naye, Afisa Uhifadhi Mwandamizi Apaikunda Mungure alisema, "ni zaidi ya miaka 2 TANAPA imeendelea kutangaza vivutio vyake visiwani humo na sasa matunda yameanza kuoneka kwa kupokea wageni wengi kutoka Zanzibar wakitembelea Hifadhi za Taifa zilizoko Kusini mwa Tanzania".
Mbali na kutangaza vivutio na fursa za uwekezaji pia, TANAPA inaendelea kuboresha miundombinu ikiwemo malazi, barabara na Viwanja vya ndege ili kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea hifadhi hizo zilizojaliwa kuwa na sifa za kipekee.