NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
BARAZA la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limepanga kuzisimamia mamlaka za majiji na manispaa kwa lengo la kuweka mikakati ya kuzigeuza taka ngumu kuwa fursa ya ajira ambapo inakadiriwa kuwa mkoa wa Dar es Salaam unazalisha zaidi ya tani 350000 ambapo zikifanyiwa kazi zitageuka kuwa fursa.
Akizungumza leo Februari 5,2024 Jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Sayansi ya Mazingira (CSE) cha nchini India kuhusu udhibiti wa taka ngumu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Semesi amesema kuwa taka ngumu zinaweza kutumika kuzalisha nishati na kuwakomboa wananchi wengi kiuchumi na amebainisha kuwa kituo cha CSE cha India tayari kimetengeneza mwongozo wa namna ya kuzitumia taka hizo kama rasilimali.
“Taka ngumu kwenye manispaa zetu Tanzania unaendelea kuongezeka kutokana na wingi wa watu na shughuli za binadamu kwa hiyo tunapaswa kuangalia namna ya kutumia taka ngumu kama fursa na tukifanikiwa kwenye hili tutayaweka mazingira yetu safi,”Dkt. Immaculate amesema.
Amesema kuwa kuna umuhimu wa kukusanya takwimu ya taka zinazozalishwa kwenye maeneo mbalimbali nchini na namna zinavyotunzwa ili ziwe fursa kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali hali ambayo itasiadia kuweka mazingira katika hali ya usafi.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Tafiti za Maizngira (NEMC), Dk. Menan Jangu amesema kuna umuhimu wa kuboresha mifumo ya udhibiti wa taka ngumu ambazo nzimekuwa chanzo cha uchafuzi wa mazingira nchini.
Aidha amesema kuwa serikali kwa kushrikiana na wadau wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali na kwa kushirikiana na Kituo cha CSE cha India wanaweka mikakati ya kuhakikisha taka ngumu zinakuwa fursa.
Pamoja na hayo ameeleza kuwa kwa ushirikiano na kituo Cha Sayansi na Mazingira (CSE) India wamefanya mambo mengi kwenye usafi wa ziwa Victoria ambalo awali lilionekana kuwa hatarini kutokana na ongezeko la uchafuzi unaotokana na taka ngumu.
“Tatizo letu kwa sasa hatuna takwimu sahihi kuonyesha kwamba kwenye maeneo yetu tunazalisha taka kiasi gani, za aina gani na zinakwenda wapi lakini ushirikiano na kituo cha CSE tumejitahidi kufanya kazi kupunguza tatizo hili,” Dkt. Immaculate ameeleza