Breaking

Monday, 26 February 2024

Kiwanda cha Elsewedy pelekeni soko la EAC, SADC na AFCFTA

Serikali imekishauri Kiwanda cha kuzalisha nyaya za umeme pamoja na transfoma cha Elsewedy kuhakikisha inapeleka bidhaa zake katika masoko ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na hata katika Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ili kukuza uchumi wa nchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameyasema hayo Februri 26, 2024 alipofanya ziara katika Kiwanda hicho kilichoko eneo la Kisarawe 11, Kigamboni Dar es Salaam kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji na kusikiliza changamoto zao

Alisema kiwanda hicho kilifunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kinazalisha bidhaa mahsusi kwa ajili ya kwenda nchi za Kenya, Rwanda, Afrika Kusini na hata Demokrasia ya Kongo jambo ambalo lina mafanikio makubwa kwa Watanzania.

“Mmeanza kwa nchi tatu tuu bado kuna ziada, ukifika Burundi wanaendelea kujenga sana nchi yao, tushirikiane tufikie hata soko la Uganda tupeleke bidhaa zetu kwa pamoja,” alisema Dkt Kijaji.

Alisema katika kufanikisha hiko Wizara yake iko tayari kushirikiana na kiwanda hicho ili kukiwezesha kuuza bidhaa zake katika masoko hayo kwa kufuata vigezo vilivyopo na kutumia fursa zilizopo ipasavyo katika nchi zote 54 za Afrika.

Vilevile Dkt Kijaji amesema milango iko wazi kwa wawekezaji wengine wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini katika fursa mbalimbali za kuongeza uzalishaji kwenye viwanda na kwamba kama zipo changamoto zibadilishwe kuwa fursa ili kufanya kazi na kuendelea kutengeneza ajira

Aidha amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya biashara kwa kuondoa vipingamizi vya biashara kwa kiwango kikubwa na vilivyobakia vinaendelea kufanyiwa kazi .

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Elsewedy kwa EAC,Ibrahim Qamar alisema kiwanda hicho kilichoajiri vijana wa kitanzania zaidi ya 200 kilianzishwa ili kuifanya Tanznaia kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa hizo kwa afrika mashariki na Afrika kwa ujuml alakini pia hata kupenya katika masoko mbalimbali duniani.

Naye Mtaalamu wa Logistiki kiwandani hapo Ishaka Ridhwan amesema amefanikiwa kufikisha bidhaa katika nchi za Kenya, Rwanda Burundi na tayari kwa Kenya wamepeleka zaidi bidhaa za gharama ya dola za Kimarekani 10,000 kwa mwaka 2023.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages