Serikali imetoa wito kwa Watanzania kuwekeza zaidi katika viwanda vya maziwa nchini kutokana na kutolewa kwa kodi nyingi katika viwanda vya bidhaa hiyo pamoja na kuwepo kwa soko la ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe Februari 7, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Tabora, Mhe. Jacqueline Kainja, lililohoji Mpango wa Serikali kutenga fedha ili kuanzisha viwanda vya maziwa ili kuwaondolea wafugaji adha ya kupoteza maziwa.
“Ni kweli kuna upotevu wa maziwa kwa Mkoa wa Arusha na Mikoa mingine, Mkakati wa Serikali ni kuja na uwekezaji katika utunzaji ambao utasaidia viwanda kupata maziwa katika ubora wake, mpaka sasa viwanda bado vinazalisha chini ya uwezo wake kwa kuwa kuna upotevu na havipati malighafi ya kutosha". Amebainisha Kigahe.
Kigahe pia amebainisha Mkakati mwingine wa kuwasaidia wafugaji wasipoteze maziwa kuwa ni kuhakikisha wafugaji wanaingia mikataba ya ununuzi wa maziwa na wenye viwanda.
Wakati huo huo, akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum. Zaytun Seif Swai (CCM) aliyetaka kujua mkakati wa kufufua viwanda vilivyotelekezwa vikiwemo viwanda vya general Tyre, KiliTex na vya kusindika mazao, Kigahe amesema Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imepitia na kufanya tathmini ya namna ya kuvifufua viwanda vilibinafsishwa, vilivyotelekezwa na vinavyofanya kazi ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa tija.
Vilevile Kigahe amesema Serikali inaendelea na mazungumzo na wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea hususani mkoani Mtwara wakati akijibu swali la nyongeza la Mhe. Tunza Malapo (Chandema), aliyetaka kujua Mkakati wa Serikali wa kujenga kiwanda cha mbolea mkoani Mtwara,
“Mtwara ni eneo mahususi za viwanda vitakavyokuwa vinatumia gesi asilia kujiendesha, na kwa sasa tunaendelea na mazungumza na wawekezaji ambao wanaonesha nia ya kuwekeza katika viwanda vya mbolea hususani Mkoa wa Mtwara.”