Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wao katika nyanja ya biashara na uwekezaji na kuingia mikubaliano kwa pamoja kama EAC na Jumuiya nyingine za kikanda na kimataifa ili kukuza biashara na kuimarisha ushindani wa EAC katika soko la dunia.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) alipokuwa akiongea na vyombo vya habari mara baada ya kushiriki Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Kisekta wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) uliofanyika Februari, 9, 2024 jijini Arusha, Tanzania.
Aidha, amebainisha kuwa Nchi hizo zimekubaliana kusaidia sekta binafsi kukua kwa kuondoa vikwazo vya kibiashara vikiwemo vikwazo vya vikodi na visivyo vya kikodi pamoja na kuboresha miundombinu katika maeneo ya mipaka ili kuimarisha sekta hiyo ambayo ina nafasi muhimu katika maendeleo ya uchumi wa EAC.
"Makubaliano mengine ni pamoja na kuhakikisha biashara zetu zinafanyika kwa haki sawa na ndio maana tuna Tume ya Ushindani (FCC) ambayo inahakikisha wafanyabiashara nchini kutoka nchi za wenzetu wanafanya biashara kwa uhuru na kwa haki lakini pia tunahamasisha kuhusu ubora ndio maana tulikuwa na Shirika la viwango Tanzania (TBS) ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na kuuzwa EACi zinazingatia ubora." Amesema Exaud Kigahe
Vilevile Kigahe amebainisha kuwa Tanzania inatarajia kuuza bidhaa zaidi nje ya nchi mwaka huu 2024/2025 kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya kilimo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao na hivyo kuchochea mauzo ya nje.
Naye Mwenyekiti wa Mkutano huo na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Sudan Kusini Mhe. William Anyuon Kuol amesema pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa sekta bianfsi kuanzia wajasiliamali wadogo na wakubwa zinatakiwa kupewa nguvu katika maeneo ya viwanda na uwekezaji.
Mkutano huo wa 43 wa Mawaziri pia umezingatia tathimini ya kikanda kuhusu mafanikio ya eneo moja la forodha, pamoja na ripoti ya hali ya utekelezaji wa mfumo wa kielekroniki wa kufuatilia mizigo. Maazimo ya kikao hiki yatawafikia wakuu wanchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kufanyiwa maamuzi.