Breaking

Thursday, 22 February 2024

KATIBU MKUU LUHEMEJA ATOA SIKU 100 PSSSF KUKAMILISHA AWAMU YA PILI UJENZI KIWANDA CHA BIDHAA ZA NGOZI KILIMANJARO

Na. Mwandishi wetu - Kilimanjaro
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa siku 100 kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Wafanyakazi wa Umma (PSSSF) Ndg. Abdul-Razaq Badru kuhakikisha Awamu ya Pili ujenzi wa kiwanda cha kuchakata Bidhaa za Ngozi Kilimanjaro unakamilika na kuanza kufanya kazi ifikapo Julai 2024.
Agizo hilo amelitoa leo Februari 22, 2024 alipo fanya ziara ya kukagua ujenzi katika kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro International Leather Industries Ltd (KLICL) ikiwa ni sehemu ya kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na serikali kupitia Ofisi hiyo.
Mhandisi Luhemeja amesema kukamilika kwa kiwanda hicho kutaongeza thamani ya zao la ngozi ghafi, kufungua fursa za soko la uhakika la Ngozi kutoka kwa wafugaji, kuongeza ajira kwa vijana na mapato ya fedha za ndani na za kigeni.


Aidha, amefurahishwa na ubora wa bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo na kutoa wito kwa watanzania kuwa na tamaduni za kuthamini bidhaa zinazo zalishwa nchini.


Awali akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Ndg. Abdul-Razaq Badru amesema amepokea maagizo hayo ya Katibu Mkuu Mhandisi Luhemeja na kuahidi kuwa PSSSF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi kama ilivyo elekezwa ili watanzania waanze kunufaika na mradi huo.


Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Mhandisi Saiba Edward amesema mradi huo pamoja na mambo mengine, utaongeza kipato kwa wakazi wa Kilimanjaro na Mikoa jirani kupitia fursa za uzabuni, uwakala na usambazaji wa bidhaa.


Kwa upande wake Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Magereza Frank Mwakijungu amebainisha kuwa Magereza ni mbia wa utekelezaji wa Mradi huo hivyo watasimamia ujenzi wa kiwanda hicho ili kikamilike kwa wakati kwa manufaa ya watanzania.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemaja (kushoto) akikagua bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro International Leather Industries Ltd (KLICL) leo Februari 22, 2024 ikiwa ni mwendelezo wa kukagua miradi inayotekelezwa na serikali kupitia Ofisi hiyo.




















Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages