Breaking

Saturday, 24 February 2024

KAMATI YA BUNGE YAITAKA SERIKALI KUPANUA WIGO WA UTOAJI HUDUMA MNH MLOGANZILA

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI imeitaka Serikali kupanua wigo wa utoaji huduma katika hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwani hospitali hiyo bado inaeneo kubwa ambapo kuna takribani ekari 3800.

Akizungumza leo Februari 24, 2024 wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ya kutembelea hospitalini hapo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa kujenga hospitali hiyo ambapo pia kuna kituo kingine cha utafiti wa magonjwa ya moyo ambacho kimejengwa katika eneo hilo.

"Tunahitaji upanuzi wa huduma za magonjwa ya moyo, upanuzi wa huduma za saratani, upanuzi wa huduma za magonjwa mengine ya mifupa na mfumo wa ubongo ili wananchi waweze kupata huduma bora na rahisi kwa wepesi zaidi hapa nchini". Amesema Dkt. Ndugulile.

Aidha Dkt. Ngugulile amesema kuna fedha wameambiwa zimepatikana, ujenzi unashindwa kuendelea kwasababu masuala ya umiliki wa ardhi hayajakamilika hivyo wameitaka serikali, Wizara ya afya na Wizara ya Elimu kukaa pamoja ili kuweza kufikia muafaka ili uwekezaji uweze kufanyika kwasababu wananchi wanahitaji huduma bora zaidi na eneo hilo linatosha kwa matumizi yote ya elimu pamoja na huduma za afya.

Pamoja na hayo Kamati hiyo imeridhishwa na hali ya utoaji huduma katika hospitali hiyo kuanzia kwa wafanyakazi, vifaa bora na vya kisasa vya kutolea huduma ambapo pia mazingira yanaridhisha na wagonjwa wanahudumiwa vizuri.

Hata hivyo ameipongeza Serikali kwa kuboresha huduma za afya nchini kwani kwasasa asilimia 90 ya wagonjwa ambao walikuwa wanakwenda nje ya nchi kutibiwa kwasasa wanatibiwa hapa nchini na tumeanza kupata wageni kutoka nje ya nchi kuja kupata huduma nchini.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye sekta ya afya hasa kwenye miundombinu, teknolojia ya afya pamoja na kwenye wataalamu, kwani kwasasa tunawataalamu wa kutosha kwenye masuala mbalimbali ya utoaji huduma za afya hapa nchini.

Amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wamezalisha bilioni 8 kwa kufanya tiba urembo ambapo pia wameboresha maeneo mengi huduma ikiwemo mazingira mazuri ya utoaji huduma, ununuzi wa vifaa bora na vya kisasa pamoja na kuboresha chumba cha kuhifadhia maiti.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages