Breaking

Sunday, 7 January 2024

WANANCHI, JASIRIAMALI IRAMBA WAPEWA BURE MITUNGI YA GESI YA ORYX 700 PAMOJA NA MAJIKO YAKE

Na Mwandishi Wetu, Iramba

KAMPUNI ya Oryx Gas Tanzania imegawa bure mitungi ya gesi 700 yakiwa na majiko yake yenye jumla ya thamani ya Sh.milioni kwa wananchi wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida kwa lengo la kuunga mkono mkakati wa Serikali wa kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yanapewa nafasi ili kuepusha madhara yanayotokana na utumiaji wa kuni na mkaa.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa mitungi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amewaomba wananchi kuendelea kuyatazama matumizi ya gesi ya kupikia nyumbani kuwa huduma muhimu katika kulinda afya ya jamii.

“Oryx Gas tunaamini ukipika kwa kutumia gesi, inaleta maendeleo mengi katika jamii.Pia kupika kwa gesi ya Oryx ni kulinda mazingira kwa kuacha kukata miti.Zaidi ya yote ni kulinda afya ya wanawake kwa kuwaepusha kuvuta moshi unaoathiri mapafu na afya yao.”

Ameongeza kwa miaka mingi Oryx Gas imekuwa kampuni kiongozi katika kukuza matumizi ya gesi nchini huku akifafanua kuanzia Julai mwaka 2021 wamekuwa mstari wa mbele kutekeleza maelekezo ya Serikali waliyopokea kutoka kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa ifikapo mwaka 2032 asilimia 80 ya Watanzania itumie nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.

Amesema kupitia mipango hiyo, Oryx Gas inataka kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa.Amemshukuru Mbunge wa Iramba Dk. Mwigulu Nchemba kwa kuwa balozi mzuri wa kuleta maendeleo kwa wanawake na jamii kwa ujumla kwa kuiunga mkono Oryx Gas katika mpango wa matumizi ya nishati safi mkoani Singida.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Seleman Mwenda amesema wamegawa mitungi hiyo kwa baba na mama lishe ikiwa ni sehemu kumuunga mkono Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuhimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.

Amesema kupika kwa gesi kunasaidia kutunza mazingira pamoja na afya hasa kwa wanaojihusisha na shughuli za upishi huku akifafanua wamegundua misitu inateketea kwa sababu ya matumizi ya kupikia,”amesema.

Aongeza athari nyingi ambazo wanazipata baba na mama lishe zinatokana na mkaa pamoja na kuni na hivyo kuathiri afya zao.

“Katika kuunga mkono juhudi za Serikali tuliamua kuwasiliana na Oryx na tunashukuru wameitikia mwito uliopelekekwa na Mbunge wetu na Waziri wa Fedha Dk.Mwigulu Nchemba,”amesema Mwenda wakati wa ugawaji wa mitungi hiyo akimwakilisha Dk.Mwigulu.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Seleman Mwenda( wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Benoite Araman(wa pili kulia) wakimkabidhi mtungi wa gesi ya Oryx Ezekiel Daghora (katikati) ambaye ni Baba Lishe wakati wa tukio la ugawaji mitungi 700 kwa wananchi wa Wilaya ya Iramba wakiwemo wajasiriamali

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages