Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imekamilisha ujenzi wa vituo 30 vya huduma kwa jamii( Public Sanitary Service Point) katika wilaya zote tano za Mkoa wa Dar es salaam huku soko la kuku Manzese wakiwa wanufaika wa kwanza tangu kukamilika kwa mradi.
Akizungumza na wanahabari, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA Ndugu Everlasting Lyaro ameeleza ya kuwa vituo hivi vinatajwa kuwa vinara wa usafi wa Mazingira na kutoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu iliyowekwa kwa matumizi endelevu
“Vituo hivi vya jamii vinapatikana katika wilaya zote tano ambazo ni Ubungo, Kinondoni, Ilala, Kigamboni na Temeke na vimejengwa katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa wananchi hususani katika maeneo ya Masoko, stendi za mabasi pamoja na maeneo yenye mikusanyo ya watu wengi kwa lengo la kuboresha usafi wa Mazingira kwa wakazi wa maeneo hayo.
"Tumekamilisha mradi wa ujenzi wa vituo 30 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kwa awamu ya kwanza tumeanza na vyoo vitano na hapa Soko la Kuku Manzense ni wanufaika wa kwanza wa mradi huu na zote ni jitihada zinazofanywa na Mamlaka katika kuboresha usafi wa Mazingira na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko" amesema Ndugu Lyaro
Pia ameeleza kituo cha Manzense kimehusisha matundu ya choo 15 kwa upande wa wanaume na matundu 16 kwa upande wa wanawake, sehemu za kujistiri kwa kina mama pamoja na chumba maalum cha kubadilishia taulo za watoto wadogo na kubwa zaidi uwepo wa miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.
Naye, Afisa Mtendaji Kata ya Manzese Ndugu Rozina Kimario amesema wanaishukuru Serikali ya awamu ya sita kupitia DAWASA kwa utekelezaji wa mradi huu wenye manufaa makubwa kwa jamii hususani wakazi na wafanyabiashara wa eneo hili la Manzese kwani kitaenda kumaliza changamoto iliyokuwepo kwa mda mrefu ya huduma ya choo cha kisasa katika eneo hilo.
Naye, Katibu wa wafanyabiashara Soko la Manzense Mustafa Lilonge amesema mradi huo umekuwa msaada kwa wafanyabiashara na kuahidi kutoa ushirikiano kwa DAWASA na kuhimiza usimamizi wa kuvitunza ili kiendelee kutoa huduma endelevu.
" Napenda kutoa shukrani kwa Serikali yangu sikivu kwa kuona umuhimu wa kutuletea wa vyoo hivi, usimamizi mzuri wa Manispaa pamoja na uongozi wa Kata ya Manzense tumeambiwa kinaweza kuhudumia watu zaidi ya 500 kwa siku hii ni kubwa kwetu sio kwamba tulikua hatuna vyoo la hasha vilikuwepo lakini havikuwa bora kilichobaki upande wetu ni kuvitunza na kama kiongozi wa hapa naahidi kutoa ushirikiano kwenye hilo" amesema Ndugu Lilonge.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990