Breaking

Friday, 26 January 2024

MKUTANO WA PILI WA BARAZA LA WAFANYAKAZI PURA WAZINDULIWA

Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi PURA umezinduliwa leo, Januari 26, 2024 katika Hoteli ya Morena Mjini Morogoro.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na wageni mbalimbali akiwemo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Ndg. Athumani Selemani Mbuttuka ambaye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Nishati.

Wageni wengine walioshiriki tukio hilo ni Kamishna Msaidizi wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira Na Wenye Ulemavu) Ndg. Andrew Mwalwisi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini Ndg. Hery Mkunda na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Sara Rwezaula.

Akitoa neno la kumkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi PURA ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Mha. Charles Sangweni amesema kuwa tangu Mamlaka hiyo ianze kufanya vikao vya Baraza, ushirikishwaji wa wafanyakazi katika masuala mbalimbali yanayohusu Taasisi hiyo umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Ndg. Mgeni rasmi, napenda kukujukisha kuwa tangu PURA imezindua Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Wafanyakazi mwezi Novemba 2020 kiwango cha ushirikishwaji wa wafanyakazi, uwazi na utendaji kazi wa Taasisi umeimarika kwa kiasi kikubwa” alisema Mha. Sangweni.

Katika hotuba aliyoisoma kwa Niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Nishati wakati wa halfa ya ufunguzi, Ndg. Mbuttuka amesema kuwa miongoni mwa majukumu ya msingi ya Baraza ni kuhakikisha kuwa haki na wajibu wa mwajiri na mtumishi vinapewa kipaumbele katika utekelezaji wa majukumu.

Aidha, Ndg. Mbuttuka alitumia fursa hiyo kutoa wito wa wafanyakazi wa PURA kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ubunifu, weledi na kuwa watumishi wa wananchi.

“Daima tukumbuke kuwa ili utumishi wa Umma uweze kuheshimika ni wajibu wetu kama watumishi wa Umma kufanya kilicho sahihi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa. Tukumbuke kuwa sisi watumishi wa umma ni waajiriwa wa wananchi, hivyo, kwa nafasi zetu tuwatumikie wananchi” alieleza Ndg. Mbuttuka.

Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi PURA unaundwa na jumla ya wajumbe 35. Kwa mujibu wa Mkataba wa Kuundwa kwa Baraza la Wafanyakazi PURA, Mkutano huo utadumu kwa muda wa miaka mitatu, kuanzia Januari 2023 hadi Januari 2026.



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Ndg. Athumani Selemani Mbuttuka (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi PURA. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa PURA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi PURA Mha. Charles Sangweni na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini Cde. Hery Mkunda (kulia)

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Ndg. Athumani Selemani Mbuttuka (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa PURA na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi PURA Mha. Charles Sangweni (kushoto) na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini Cde. Hery Mkunda (kulia) katika tukio la uzinduzi wa Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi PURA
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages