Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imekamilisha mradi wa uboreshaji wa usafi wa mazingira katika kata ya Mwananyamala uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 230 na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kupata huduma.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika Dawati la huduma kwa wateja mtaa wa Msisiri A kata ya Mwananyamala, Msimamizi msaidizi wa mradi kutoka DAWASA , Miriam Mgata amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma ya maunganisho ya majitaka ili kuboresha usafi wa mazingira eneo la mwananyamala.
"Mradi huu ni umelenga eneo la mwananyamala kuwa safi na salama, tuna furaha kuwa mradi umekamilika na sasa ni fursa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hii, kupitia dawati hili la huduma kwa wateja ambalo lipo hapa ofisi ya mtendaji wa kata ili kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi na kuwahudumia" ameeleza ndugu Mgata
Gasper Chambembe, Mwenyekiti wa mtaa wa Msisiri A, ameipongeza DAWASA kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi na kuwahasa wananchi wa eneo lake ambao bado hawajajiunga na huduma hii kujitokeza kwa wingi na kupata huduma waliyoingoja muda mrefu.
Ndugu Rehema Mtanga, mkazi wa mtaa wa Msisiri A ameishukuru DAWASA kuwatembelea na kuwapatia elimu juu ya usafi wa mazingira na kuahidi ushirikiano na kuhamasisha wengi zaidi kujitokeza kujiunga kwenye mfumo.
Mradi wa usafi wa mazingira Mwananyamala umetekelezwa ukihusisha kazi mbalimbali ikiwemo uchimbaji na ulazaji wa bomba za inchi 8 kwa umbali wa kilomita 1.6 pamoja na ujenzi wa chemba 32 za kukusanya majitaka na utahudumia kaya zaidi ya 100 katika mitaa ya *Msufini, barabara ya Dunga, Mwananyamala Kanisani, na maeneo ya jirani na kata ya Mwananyamala*
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990