Breaking

Thursday, 4 January 2024

MAANDALIZI UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI BANGULO YAANZA





Maandalizi ya awali ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Bangulo utakaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wenye gharama ya Shilingi Bilioni 40 yameanza rasmi kwa Mkandarasi wa mradi kampuni ya SINOHYDRO kutoka China kuanza hatua ya maandalizi ya kukusanya vifaa vya ujenzi.

Ikiwa ni miezi miwili sasa tangu kusainiwa kwa mkataba wa utekelezaji wa mradi na kukabidhi eneo la ujenzi kwa Mkandarasi, utekelezaji wa mradi huu unalenga kunufaisha wananchi 450,000.

Akielezea hatua mbalimbali zilizofikiwa za utekelezaji wa mradi Meneja wa usimamizi wa mradi kutoka kampuni ya SINOHYDRO ya China Ndugu Xie Zhen amesema kuwa kazi za awali zilizofanyika ni pamoja na utafiti wa udongo kubaini ubora wa udongo sehemu itakayojenga tenki la maji Bangulo pamoja na kituo cha kusukuma maji.

"Pia kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na kuanza kwa ujenzi wa nyumba ya Mkandarasi ya kuweka vifaa na malighafi za ujenzi ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huu utakaokuwa suluhu kwa wananchi wengi wa maeneo husika," amesema.

Mradi wa maji Bangulo umesanifiwa na kutekelezwa na DAWASA katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza utekelezaji wa mradi umehusisha ujenzi wa kituo cha kusukuma maji, kazi ya ulazaji wa bomba la chuma la inchi 28 kwa umbali wa kilomita 11.052 kutoka kwenye kituo cha kusukuma maji Kibamba mpaka Bangulo. Pia ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji la ukubwa wa lita milioni 9.

Pia awamu ya pili ya mradi itahusisha ujenzi wa matoleo 18 ya kutoa maji kutoka kwenye bomba kuu la kusafirisha na kusambaza maji, uchimbaji na ulazaji wa bomba za kusambaza maji za ukubwa wa inchi 10 kwa umbali wa kilomita 2.9, pamoja na uchimbaji na ujenzi wa mtandao wa kusambaza maji kwa umbali wa kilomita 28.14.

Nae mkazi wa mtaa wa Hali ya hewa Ndugu Peter Mwakyosa amesema shida ya maji kwenye eneo lao ni kubwa kiasi cha kununua maji tena kwa gharama kubwa.

Amesema kuwa kwa muda mrefu sasa, hawajawahi kuona majisafi ya bomba na wamekuwa wakitumia maji ya visima na ya madumu ambayo mengi sio salama kiafya.

Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuona haja ya kufikisha huduma ya maji kwenye eneo lao na kutaja mradi huu utakuwa mkombozi mkubwa.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages