Breaking

Friday, 12 January 2024

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE ARDHI, MALIASILI NA UTALII YAPONGEZA UJENZI WA MIUNDOMBINU HIFADHI YA TAIFA MIKUMI, WAMPONGEZA RAIS SAMIA.

Na. Zainabu Ally – Mikumi.

Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii imepongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kusimamia miradi ya kukuza utalii kusini mwa Tanzania (REGROW) inayotekelezwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi.

Akizungumza mara baada ya Kamati hiyo kufanya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa kiwanja cha ndege kikubwa kinachojengwa katika Hifadhi ya Taifa Mikumi pamoja na kutembelea vikundi vya Kijamii (COCOBA) vinavyowezeshwa na Mradi wa REGROW, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Timotheo Mnzava amepongeza mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo yenye lengo la kukuza Sekta ya Utalii kwa Ukanda wa Kusini.

"Kwa niaba ya Kamati, nichukue fursa hii kuipongeza Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na timu nzima inayosimamia utekelezaji wa miradi hii, leo tumekuwa na muda wa kutosha kujionea utekelezaji wa Miradi ya REGROW kwenye eneo la Hifadhi ya Taifa Mikumi, na kwakweli tumeona kazi nzuri inayofanywa kupitia mradi huu”. Alisema Mhe. Mnzava

Aidha, Mnzava alitoa wito kwa kuwataka wasimamizi wa miradi hii kuendana na kasi katika kuchagiza maendeleo ya ukuaji kwa sekta ya utalii kwa kuongeza nguvu na kasi katika kuwasimamia wakandarasi ili kukamilisha miradi yote kwa muda uliopangwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake kuhakikisha sekta ya utalii inakua na kupiga hatua kubwa katika kuchangia uchumi kwa taifa kupitia ongezeko la watalii.

Mhe. Kitandula ameihakikishia Kamati kwamba, Wizara itaendelea kupokea maelekezo na kuyafanyia kazi kwa wakati ili kuhakikisha miradi inakamilika ndani ya muda uliokusudiwa.

Naye, Kamisha Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Mashariki Massana Mwishawa, wakati akiupokea ugeni huo alipongeza kazi kubwa zinazofanywa na Serikali chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uboreshaji mkubwa wa Sekta ya Utalii chini ya Taasisi zake ikiwemo TANAPA, ambapo alisema uboreshaji wa miundombinu Kusini mwa Tanzania kupitia mradi wa REGROW utasaidia kufungua milango ya utalii.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo iliyoambatana na Naibu Waziri wa maliasilia na Utalii, Makamishna, maafisa na askari wa uhifadhi kutoka Hifadhi ya Taifa Mikumi walitembelea katika vijiji jirani ambavyo ni wanufaika wakubwa wa Mradi wa REGROW. Miongoni mwa kikundi kilichotembelewa ni cha Masai Bomba kinachojihusisha na shughuli za utalii wa kiutamaduni.

Kiwanja cha ndege kinachojengwa Hifadhi ya Taifa Mikumi kitakuwa na uwezo wa kutua ndege zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 30-50 kwa wakati mmoja. Maendeleo haya yatasaidia kukuza utalii kwa kuongeza idadi ya wageni na mapato na kufikia malengo ya serikali ya kukusanya dola za kimarekani bilioni 6 na watalii milioni tano ifikapo 2025.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages