Breaking

Tuesday 16 January 2024

DAWASA YABAINISHA MIKAKATI KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO



Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert John Chalamila amewataka watendaji wa Serikali katika Mkoa wa Dar es salaa kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko huku akiitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji na usafishaji mifumo ya majitaka kwa wakati.

Mhe. Chalamila amesisitiza kila Mtendaji kushiriki katika kutimiza majukumu yake na kuhakikisha mkoa wa Dar es salaam kutokuingia kwenye orodha ya mikoa iliyoathiriwa na kipindupindu Nchini.

"Kama takwimu zinavyoonyesha na Mganga mkuu pia ametuthibitishia kuwa ugonjwa huu ulishawahi kuwepo Dar es salaam na hali ilivyokua ngumu kwenye kuudhibiti, kwa mantiki hiyo tuhakikishe ugonjwa huo haupenyi kwenye mipaka ya Mkoa wetu." amesema Mhe. Chalamila

Mhe. Chalamila ametoa maagizo kwa watendaji ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Mitaa kusafisha maeneo mbalimbali kwa kufanya usafi kila wiki, kuhifadhi taka sehemu stahiki pia kutumia magari ya kuzolea taka ili kuzuia kuzagaa kwa takataka katika mazingira ya watu.

Pia, Mhe. Chalamila ametoa agizo kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kufanya maboresho kwenye miundombinu ya majitaka hasa kwenye maeneo yenye msongamano wa watu wengi , na kupanua mtandao kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA , Mhandisi Christian Christopher ameeleza jitihada zinazoendelea kufanywa na Mamlaka katika utunzaji wa Mazingira ikiwa ni pamoja na uwepo wa magari na mitambo ya kisasa ya uondoshaji wa majitaka inayopatikana muda mrefu na upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo mengi.

Pia, Mhandisi Christopher ameongeza kuwa kwa upande wa huduma ya majisafi jitihada zinazofanyika ni kuhakikisha maji yanayoenda kwa wananchi yanatibiwa kwa kiwango sahihi cha dawa na kupimwa ili kuhakiki ubora wake.

Kikao kazi hicho kimewakutanisha watendaji kutoka Wilaya, Kata zilizopo mkoani Dar es salaam pamoja na watendaji kutoka Taasisi za Serikali na Taasisi binafsi.




Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages