*Serikali yaunda kikosi kazi cha ukaguzi wa kushtukiza
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) imetangaza kuanza kuwashughulikia wazalishaji na wauzaji wa vyakula vya mifugo wasiofuata sheria na kanuni zinazoongoza utekelezaji wa shughuli hizo.
Hayo yamesemwa Desemba 02, 2023 na Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo Dkt. Stella Bitanyi alipokuwa akitoa taarifa fupi ya yaliyobainika wakati wa operesheni maalum iliyoendeshwa na timu ya wataalam kutoka ofisini kwake kwa kushirikiana na wakaguzi wa vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambao walifanya ukaguzi katika viwanda vinavyozalisha na maduka yanayouza vyakula hivyo katika mikoa ya Dar-es-salaam na Pwani kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 01, 2023.
Dkt. Bitanyi amewataka wazalishaji wote wa vyakula vya mifugo hapa nchini kuzalisha vyakula vyenye uwiano sahihi wa viinilishe vinavyohitajika kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa na mamlaka ya kuthibitisha ubora wa vyakula hivyo (TBS) na viwango vya kimataifa kwa wale watakaohitaji kusafirisha nje ya nchi.
“Lakini pia tunawaagiza kila kundi la chakula wanalozalisha wahakikishe sampuli yake inapelekwa kwenye maabara kuu ya veterinari ambao ndio wenye ithibati ya kitaifa ya kuchambua vyakula vya Mifugo ili waweze kuthibitisha na kutoa vyeti vya ubora” Amesema Dkt. Bitanyi.
Aidha Dkt. Bitanyi amewataka wazalishaji kuhakikisha wanapima malighafi zote wanazotumia kutengeneza vyakula vya mifugo huku pia akiwaelekeza kusajili Taasisi na mahali wanapozalishia vyakula hivyo.
“Tunafahamu kwamba usajili ni kila mwaka hivyo wale ambao hawajasajiliwa wafanye hivyo na wale ambao tayari wameshasajiliwa waendelee kuhuisha usajili wao kupitia tovuti ya Wizara ambako watapata maelekezo yote ya kufanya mazoezi hayo” Ameongeza Dkt. Bitanyi.
Akitoa malekezo upande kwa wa wauzaji wa vyakula hivyo, Dkt. Bitanyi amewataka kuhakikisha wananunua vyakula vyao kutoka kwa wazalishaji waliothibitishwa kwenye viwango vya ubora kwa kila kundi la chakula wanalotaka kununua kwa wazalishaji hao.
Akizungumza mara baada ya kutembelewa na timu ya wataalam hao mmoja wa wazalishaji wa vyakula vya Mifugo kutoka mkoani Pwani Bw. Samson Maro ameipongeza Serikali kwa kufanya zoezi hilo mara kwa mara ambapo ameahidi kuyafanyia kazi yale aliyoshauriwa na wataalam hao.
Naye mmoja wa wauzaji wa chanjo na Vyakula vya kuku na bata kutoka mkoani humo Bi. Domitila Melisa amewaeleza wataalam hao namna anavyowasaidia wafugaji waliopo kwenye eneo lake kwa kuwapa elimu na ushauri kuhusu aina ya chakula wanachopaswa kupewa ndege hao kulingana na umri walionao.
Akizungumzia hali yake ya ufugaji kabla ya kupewa elimu inayohusu vyakula vya mifugo, Mfugaji wa kuku kutoka Kibaha mkoani Pwani Bi. Mwajuma Mwami amesema kuwa alikuwa akinunua vifaranga na chakula cha kuku wake kwa kubahatisha jambo lililokuwa linasababisha vifo vya mara kwa mara vya vifaranga hao ambapo ameiomba Serikali kufanya zoezi la ukaguzi na uhakiki wa viwanda na maduka ya vyakula vya mifugo kuwa endelevu.
Uzalishaji wa vyakula vya mifugo nchini unasimamiwa na sheria ya Nyanda za malisho na chakula cha mifugo ya mwaka 2010 pamoja na kanuni zake zilizoandaliwa mwaka 2013, ambapo kwa pamoja vinawataka wazalishaji na wauzaji wa vyakula hivyo kuhakikisha wanyama wanapata vyakula bora ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao yao.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi akitoa taarifa fupi ya operesheni ya siku 2 ya ukaguzi wa viwanda na maduka yanayouza vyakula vya Mifugo ofisini kwake jijini Dar-es-Salaam Desemba 02,2023.
Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) Dkt. Zacharia Makondo (kulia) akimuelimisha Muuzaji wa vyakula vya Mifugo Bi Domitela Melisa (katikati) muda mfupi baada ya kufika dukani kwake Wilayani Kibaha Desemba 02, 2023 ikiwa ni sehemu ya Operesheni ya ukaguzi wa viwanda na maduka ya vyakula vya Mifugo iliyofanywa kwa muda wa siku 2 na Wakala hiyo kwa kushirikiana na wakaguzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye mikoa ya Dar-es-Salaam na Pwani. Kushoto ni Meneja wa Maabara kuu ya Veterinari Dkt. Geofrey Omarch.
Muuzaji wa vyakula vya Mifugo Kutoka Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Bi Domitela Melisa (Kulia) akitoa ushauri kuhusu lishe ya kuku kwa mmoja wa wafugaji aliyefika dukani kwake (kushoto), wanaoshuhudia katikati ni Meneja wa Maabara kuu ya Veterinari nchini Dkt. Geofrey Omarch na Mkaguzi wa vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Theodata Salema waliofika dukani hapo Desemba 1,2023 kukagua namna huduma ya vyakula vya Mifugo inavyotolewa.
Meneja wa Uzalishaji Chakula cha kuku wa kiwanda cha Interchick kilichopo mbezi jijini Dar es Salaam Bw. Dickson Gerald (wa tatu kutoka kushoto) akitoa maelezo ya namna kiwanda chao kinavyofanya kazi kwa wakaguzi wa vyakula vya mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) waliofika Kiwandani hapo Novemba 30, 2023 ikiwa ni sehemu ya operesheni yao ya siku 2 ya ukaguzi wa viwanda na maduka ya vyakula vya Mifugo kwenye mikoa ya Dar-es-Salaam na Pwani.