Breaking

Tuesday, 12 December 2023

UREJESHAJI MIUNDOMBINU YA BARABARA KATESH WAFIKIA ASILIMIA 75

Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amesema hadi sasa urejeshaji wa miundombinu ya barabara na makalvati iliyokuwa imeharibiwa na maporomoko ya matope na mawe yaliyotokea Disemba 3, 2023 kwenye mji wa Katesh wilayani Hanang mkoani Manyara umefikia asilimia 75.

Kasekenya amesema hayo leo Disemba 12, 2023 mkoani Manyara mara baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa kazi hizo zinazofanywa na Wakala ya Barabara (TANROADS) wakishirikiana na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

"Hadi sasa tumefikia karibu asilimia 75 ya kuirejesha Katesh katika hali yake na tutakachofanya kabla ya kuondoka tutakuwa tumehakikisha tumesafisha barabara zote na kuzirudisha katika hali yake ya awali kama tulivyokuwa tumeagizwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan", amesema Kasekenya.

Kasekenya ameongeza kuwa mitambo na magari imeshafika eneo la Katesh ambapo kuna magari 32 yenye uzito wa tani 13, vijiko 12, doza 3, magari ya kishindilia barabara miwili, mitambo ya kubeba matope (roller) miwili, na mitambo yote hiyo inaendelea kufanya kazi usiku na mchana.

"Ninaposema magari yenye uzito wa tani 13 na yale yenye uwezo wa kubeba magunia 130 kwa wakati mmoja na mpaka sasa magari hayo yameweza kubeba Trip za tope na mawe zaidi ya 4,000 na kazi bado inaendelea", amefafanua Kasekenya

Amesema Wizara hiyo kupitia Wakala hizo wanaendelea kufungua barabara za mitaa kwa ajili ya kuhakikisha njia zinafunguka kwa kutoa mawe na magogo ili kuhakikisha kama kuna mali za watu zilisalia katika makazi yao wanaweza kuingia na kufanya usafi.

"Kwahiyo kazi kubwa ambayo tunafanya sisi Wizara, TANROADS na TARURA ni kurudisha maeneo yote ya mitaa, vichochoro na kusafisha eneo la soko na kuwarudisha wale waliokuwa wanafanyabiashara au waliokuwa wanaishi waweze kuishi kwenye nyumba zao na tumejipangia mpaka kufikia kesho tuwe tumefikia walau asilimia 95", amesisitiza Eng. Kasekenya.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa mbali na Serikali kurejesha miundombinu pia imeendelea kuwa bega kwa bega na Wananchi sambamba na kutoa maagizo kwa Wataalamu wa Satellite kuanza kuangalia Kaya zote na kuona zipi zimeathirika zaidi huku ikiendelea kutoa msaada zaidi.

"Kiu ya Mhe. Rais ni kuona wale ambao wamepoteza makazi tunaipata hesabu yao vizuri ili Serikali ianze mchakato wa makazi mapya kwa waathirika hao", amefafanua Mhe. Jenista.

Aidha, Waziri Jenista ametoa shukrani zake kwa juhudi kubwa za uokoaji lakini pia kwa ushirikiano wa Viongozi wote wa Mkoa, Wilaya na Serikali za mitaa kwa kuendelea kutatua changamoto sambamba na kuwapatia mahitaji muhimu ya kibinadamu waathirika wote wa maporomoko ya matope na mawe waliopo kambini lengo likiwa ni kurejesha faraja tena," amesema Jenista.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Festo Dugange amesema kuwa waathirika wa Maafa ya maporomoko ya tope 117 wameendelea kupatiwa matibabu bure tangu kutokea kwa maafa hayo hadi leo kwa gharama ya Serikali katika Hospitali ya Mkoa, Wilaya na Kituo cha Afya cha Gendabi.

"Mhe. Rais tayari amekwishaleta fedha zaidi ya Milioni 560 kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba lakini pia kununua madaawa kwa ajili ya kinga ya mlipuko wa magonjwa", amesema Dkt. Dugange.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages