Breaking

Thursday, 14 December 2023

TEC YAANZA KUWANOA WALIMU SHULE ZA KANISA KUKABILIANA MABADILIKO YA MITAALA

Na Carren Mgonja

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kupitia Idara ya Elimu kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) wametoa mafunzo kwa walimu wa shule za awali na msingi kwa shule zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki, ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa kwa ajili ya mitaala mipya iliyoboreshwa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Elimu TEC, Sista Joyce Mboya, kwa kuanza, mafunzo hayo yametolewa kwa takribani walimu 150 kutoka shule za Kanisa zilizopo chini ya Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam ikihusisha Majimbo ya Tanga, Morogoro, Ifakara, Mahenge na Dar es Salaam yenyewe na kwamba, zoezi hilo litaendelea kwenye majimbo yote nchini kupitia Majimbo Makuu.

“Tunatarajia mafunzo kama haya pia yafanyike kwenye Majimbo Makuu ya Dodoma, Tabora, Mwanza, Mbeya, Songea na Arusha ambapo matarajio hadi kufikia mwishoni mwa Januari walimu wote wawe wameshapata mafunzo haya ili wanapoanza muhula mpya wa masomo wawe tayari wamekwishajua nini kinatakiwa kufanyika kulingana na mabadiliko haya ya mitaala,” amesema Sista Mboya.

Akifungua mafunzo hayo upande wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu wa TEC, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Huduma za Jamii TEC, Padri Paulo Chobo amewataka washiriki hao kujenga umakini kipindi chote cha mafunzo kwa kuzingatia umuhimu wao kama walimu, kwamba ndiyo kiini kikubwa cha mafanikio ya mitaala hii mipya.

“Ni wazi kwamba nia ya serikali kufanya mabadiliko ya elimu ni kuwezesha wanafunzi kupata elimu itakayowajenga katika maisha wanayoendea baada ya kuhitimu, hivyo ili liweze kufanikiwa, walimu ni nyenzo na watu muhimu kwani wao ndio wanaoshusha elimu hii ya mitaala mipya kwa wanafunzi, hivyo uelewa wenu ndiyo mafanikio ya kile kinacholengwa na serikali,” amesema Padri Chobo.

Ameongeza kuwa kufuatia mabadiliko haya, Kanisa kwa nia moja limeona ni wakati mwafaka sasa kuweza kuwaandaa walimu wake ili kwa kutumia weledi wao na kwa kuongezewa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo juu ya mitaala mipya, Kanisa litaendelea kutunza heshima na sifa yake ya kutoa elimu bora yenye kuzingatia maadili na ufaulu kwa wanafunzi wake.

“Tunajua ufaulu wa shule za Kanisa ni matokeo ya sadaka kubwa inayotolewa na wote walimu na wazazi... wazazi wanajinyima na kutoa ada kwa watoto wao, lakini nyie walimu kwa namna ya pekee mnahakikisha wanafunzi wanafundishwa na kuelewa…hakika hii ni sadaka kubwa” Amesema.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mtunza mitaala kutoka mamlaka ya Elimu (TET) Steven Mwashihava, alisema kuwa ujio wa mafunzo hayo unazidi kuijengea TET matumaini zaidi kwa Shule za Kanisa ambazo zimeonyesha nia ya kwenda na kasi ya mabadiliko ya mitaala.

Mwashihava amesema kuwa pamoja na mambo mengine, katika mafunzo hayo washiriki watapata nafasi ya kupewa mbinu juu ya uchambuzi wa mitaala hiyo mipya katika ngazi ya shule za awali, shule za msingi kwa kila darasa na kuchambua mihutasari ya kila somo, lakini zaidi kuwapa washiriki mbinu za ufundishaji na maandalizi ya somo na jinsi ya kupima uelewa wa wanafunzi.

Ikumbukuwe kuwa mabadiliko ya mitaala ya elimu yametokana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alilolitoa Aprili 22 mwaka 2021 jijini Dodoma, likiwaelekeza Wizara ya Elimu kutoa elimu inayowajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri na hata kuingia kwenye soko la ajira baada ya kuhitimu wasomo yao.

Kufuatia agizo hilo, serikali kupitia Wizara ya Elimu ilianza michakato mbalimbali hatimaye serikali kuja na mabadiliko ya mfumo wa elimu ambapo Sera itakayotumika kwa sasa inatambulika kama ‘Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023’ mabadiliko ambayo pia yamekuja na maboresho ya mitaala kuanzia madarasa ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya ualimu.

Kwa mabadiliko haya elimu ya lazima kwa mwanafunzi sasa itakuwa ni miaka kumi, kianzia awali, elimu ya msingi ambayo sasa itaishia darasa la sita badala ya la saba na elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne huku mfumo wa sasa upande wa sekondari utahusisha mikondo miwili ikiwemo ya Elimu ya Jumla na Amali lakini pia mabadiliko haya yakagusa na sifa za kupokea wanafunzi wa kujiunga na vyuo vya ualimu ambapo kwa shule za msingi wanaotakiwa ni wahitimu wa kidato cha sita na kupata ufaulu mzuri, wakati upande wa sekondari ni wahitimu wa shahada ya kwanza.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages