Breaking

Saturday, 2 December 2023

TANAPA YANG’ARA TUZO ZA NBAA,

--Royal Tour yatajwa kuwa chanzo

Kaimu Kamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Juma Kuji amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani baada ya uzinduzi wa filamu ya ‘Royal Tour’ kumekuwa na mafuriko ya watalii katika maeneo tofauti ya hifadhi nchini.

Kuji ametoa kauli hiyo mara baada ya kuibuka Mshindi wa pili katika Tuzo za Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) zilizofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa imepelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la wageni na hivyo kukuza Pato la Taifa.

Akizungumzia ushindi waliopata TANAPA amesema kuwa ni chachu kwao kama Shirika na inaonesha wazi kwamba utoaji wa taarifa za fedha na utunzaji kumbukumbu hivyo Watanzania waendelee kuwa na imani na TANAPA kwa kutembelea hifadhi zilizopo nchini.

“Mwaka huu tumeibuka mshindi wa pili, mwakani tutahakikisha tunakuwa nambari moja kwani uwezo na nia tunayo ya kusimamia vizuri Maliasili za taifa”, amesema Kamishna Kuji.

“Watanzania watumie mapumziko ya mwezi Disemba kutembelea vivutio vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini, TANAPA tupo vizuri katika utoaji taarifa na utunzaji vitabu”, amesisitiza Kuji

Tuzo za uandaaji wa taarifa za fedha kwa mwaka 2023, ambazo huandaliwa na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) zimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya APC jijini Dar es Salaam.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages