Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wazalishaji wa bidhaa kupitia Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI) kuendelea kuimarisha ubora wa bidhaa wanazozalisha nchini.
Rais Samia amesema hayo leo wakati wa hafla ya utoaji Tuzo za Rais kwa wazalishaji bora (President's Manufacturer of the year Awards - PMAYA) iliyofanyika katika ukumbi wa Super Dome, Masaki.
Aidha, Rais Samia amesema serikali imeimarisha miundombinu ya barabara na bandari ili bidhaa zinazozalishwa zisafirishwe nje na kuingia nchini ili sekta ya viwanda iendelee kufanya vizuri.
Rais Samia pia amewataka wazalishaji hao kuongeza juhudi katika uzalishaji na uongezaji wa bidhaa (intermediate goods) ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Serikali inatarajia kuwasha kinu cha kwanza cha kufua umeme mwezi Januari, 2024 katika bwawa la Nyerere ikiwa ni jitihada za kuzalisha umeme wa kutosha ambao ni muhimu kwa wazalishaji.
Hali kadhalika, Rais Samia amesema mbali ya kukua kwa sekta ya utalii, jitihada nyingine inayofanywa na serikali kudhibiti dola ni kujishughulisha na kilimo hasa cha muda mfupi ambacho kinazalisha mazao kwa haraka.
Source: Ikulu Mawasiliano