CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) leo, Jumamosi tarehe 9 Desemba 2023 kimesaini Mkataba wa Hali Bora na Watumishi wake unaolenga kuboresha maslahi yao katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa Mkataba huo, Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Cde. Hery Mkunda amesema kuwa kwa mara ya kwanza Mkataba umeongeza idadi ya siku kwa mfanyakazi mwanamke atakayejifungua mtoto njiti na kufanya TUGHE kuwa Chama cha kwanza kuweka kipengele hicho katika Mkataba wake wa Hali Bora.
Cde. Mkunda amesema kuwa lengo la kuboresha kipengele hicho ni kutambua na kuthamini mchango mkubwa unaofanywa na Wanawake ndani ya TUGHE hivyo kwa kufanya hivyo kutaongeza tija na ufanisi ndani ya Chama.
Aidha ameiomba Serikali kupitia upya na kuboresha sera na sheria mbalimbali zitakazojumuisha wanawake wanaojifungua watoto njiti kama ambavyo TUGHE wameanza kufanya ili kuwapatia muda wa kuwahudumia Watoto pamoja na kuimarisha afya zao.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi Makamu Mwnyekiti wa TUGHE Taifa, Dkt. Jane Madete ameeleza kuwa amefurahishwa na uamuzi huo wa kufikia makubaliano hayo kati ya Uongozi na wafanyakazi kwani utaenda kuongeza ari ya kufanya kazi kwa bidii na kukifanya Chama kipige hatua mbele zaidi.
Nao Viongozi wa Tawi la TUGHE kwa niaba ya Wafanyakazi wamesema kuwa wamefurahishwa na mkataba huo kwani umegusa maeneo yote muhimu ambayo kwa muda mrefu walikuwa wanaomba uongozi uweze kufanya maboresho.
Mkataba huo uliosaniwa leo ni wa muda wa miaka 3 na una kipengele cha kufanyika kwa marekebisho muda wowote ambapo pande zote mbili zitaona kuna uhitaji wa kufanya hivyo. Pia Mkataba huo utawahusu Wafanyakazi wote walio katika Ajira ya kudumu na zile za mikataba ya muda maalumu na Chama.
Imetolewa na
Idara ya Habari na Uhusiano TUGHE