Breaking

Saturday, 30 December 2023

KONDOA DC NA TGNP WAJADILI MAFANIKIO YA BAJETI YENYE MTAZAMO WA KIJINSIA

 


Na Mwandishi Wetu, Kondoa

Halmashauri ya wilaya ya kondoa, mkoani Dodoma, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, imeandaa bajeti yenye mtazamo wa Kijinsia kwa kujenga miundombinu ya vyoo vya shule vyenye kukidhi mahitaji ya wasichana wanapokuwa kwenye hedhi.

Hayo yalibainishwa na Afisa Mipango wa Halmashauri, Joshua Mnyang’ali, alipokuwa akijibu taarifa ya uchambuzi wa Bajeti ya Halmashauri kwa mtazamo wa Kijinsia iliyofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Vituo vya Taarifa na Maarifa Kata ya Haubi.

“Choo tulichojenga shule ya Msingi Mwisanga na shule mpya ya sekondari ya Ntomoko, vina vyumba maalumu ya kujisitiri wasichana wanapokuwa kwenye hedhi, kichomea taka kwaajili ya kuteketeza taulo za kike ambazo zimetumika. Pia katika vyoo tunavojenga sasa, tunaweka sehemu ya haja ndogo kwa wavulana, lengo ni kupunguza msongamano kwenye vyoo, ili wanafunzi wafurahie kuwepo shuleni. Kwa kufanya hivyo tunapunguza pia utoro na kuongeza ufaulu”, alisema Mnang’ali.

Aidha naye mganga mkuu wa halmashauri, Dkt. Nelson Kimolo, amesema kwamba, Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24, imedhamiria kupunguza kabisa au ikiwezekana kutokomeza vifo vya mama na mtoto, kwa kutenga bajeti Zaidi ya shilingi Milioni 44 kwaajili ya kuwalipa madereva wa ngazi ya jamii watakaotumika kuwasafirisha Mama wajawazito kutoka zahanati kwenda Hospitali kubwa ili kurahisisha mfumo wa rufaa.

“Huu ni mradi unaojulikana kama M-MAMA ambao umeleta mabadiliko makubwa, unasaidia sana kuondoa tatizo la usafiri, magari tuliyo nayo ya kubeba wagonjwa hayatoshelezi, tumeona afadhal kuwa na utaratibu huu mpya wa kuingia mikataba na madereva waliko kwenye jamii, wahudumu wa Hospitali wawasilane nao muda wowote ili kuhakikisha Mama mjamzito anapata huduma ya haraka na kukokoa maisha yake”, alisema Dkt. Kimolo.

Awali akiwasilisha mapendekezo ya Jumla mwezeshaji wa Uchambuzi wa Bajaeti kutoka TGNP, Deogratius Temba, alisema kwamba, pamoja na halmashauri kuwa na vyanzo vichache vya mapato ya ndani, bado wamejitahidi kuangalia eneo la afya na elimu.

Temba, ameongeza kwamba, bado kuna mapengo ya kijinsia kwenye Bajeti ya Halmashauri hasa katka eneo la ustawi wa Jamii ambapo Bajeti ya kuzuia na kutokomeza Ukatili wa Kijinsia imetengwa kidogo, sambamba na Idara ya Maendeleo ya Jamii inayotakiwa kuwajibika katika uhamasishaji wa jamii kushiriki katika shughuli na maendeleo kutengewa fedha kidogo sana.

“Eneo la Ukatili wa Kijinsia, ni muhimu kuliangalia,tukiwekeza kwenye miundombinu ya elimu, alafu tusipoweka mikakati ya kuwalinda watoto wa kike na kiume wasifanyiwe ukatili wa Kijinsia na udhalilishaji wakingono, hatutapata matokeo mazuri”,alisema Temba.

Pia, eneo lingine lenye mapungufu ambalo Halmashauri imeshauriwa kuboresha na kuongeza msisistizo kwa viongozi wa vijiji na kata kuwashirikisha wananchi kwenye mchakato wa kuandaa bajeti ili waweze kuibua fursa na vikwazo katika maendeleo (O&OD) ili waweze kushiriki vizuri katika kuisimamia na kuitekeleza miradi ya maendeleo.

Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/24 imepanga kutumia kiasi cha shs.milion 440 kuboresha vyanzo vya maji, sh. Milion 3, kujenga vichomea taka katika zahanati, sh. Million 23 kujenga mashimo ya taka mbichi (placenta pit) katika zahanati na vituo vya afya, ambapo Kituo cha afya mnenia kimetengewa bajeti ya sh. Milion 35 kwa ajili ya kujenga kichomea taka na vyoo.

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), unatekeleza miradi mbalimbali katika halmashauri ya Kondoa, inayolenga kujenga uwezo wa kwa jamii kupitia Kituo cha taarifa na Maarifa, kupata uwezo wa kuchambua masuala ya Kijinsia na kushawishi kuingzwa kwa masuala ya Kijinsia katika sera, mipango na miongozo.

 Sambamba na kuwajengea uwezo viongozi mbalimbali wa Halmashauri kuhusu masuala ya Usawa wa Kijinsia na Uongozi bora na ushiriki wa wanawake katika uongozi.






Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages