Breaking

Wednesday, 13 December 2023

KINANA AZINDUA OFISI MPYA ZA CCM BUKOMBE, DKT. BITEKO ASISITIZA UMOJA WA WANANCHI






Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Komredi Abdulrahman Kinana amezindua Ofisi za kisasa za Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe mkoani Geita ambapo ujenzi wa Ofisi hizo umeenda sambamba na ujenzi wa mgahawa wa kisasa.

Uzinduzi huo umefanyika tarehe 13 Disemba, 2023 katika Ofisi za CCM Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.

Baada ya uzinduzi huo, Komredi Kinana amewapongeza Viongozi na Wanachama wa CCM wa Wilaya ya Bukombe kwa kuonesha mfano mzuri wa kukiimarisha na kukijenga Chama ambao umepelekea kuwa na Ofisi ya kisasa, Jengo zuri la mikutano, Jengo la Mapumziko na mgahawa.

Amesema kuwa, kitendo hicho ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, Sura ya Kumi, Ibara ya 246 ambayo ina orodha ya masuala mbalimbali yanayotakiwa kutekelezwa katika Miaka Mitano 2020-2025 ikiwemo kuimarisha muundo wa Chama Kitaasisi ambao unajumuisha uwepo wa Ofisi za kufanyia kazi na ukumbi wa kufanyia shughuli za Chama hivyo Bukombe wameitekeleza Ibara hiyo kwa ufanisi.

“Hamuwezi kuunda na kuimarisha muundo wa Chama kama hamna ofisi za kufanyia kazi na ukumbi wa kufanyia shughuli zenu badala yake kunapokuwa na mikutano mnakodisha kumbi nyingine na viongozi hawana ofisi; hivyo leo mmetekeleza Ibara muhimu ya Ilani ambayo tumeandaa wenyewe inayotaka WanaCCM kukiimarisha, kujijenga Chama Kitaasisi kwa kuwa na Ofisi na zana za kufanyia kazi, nawapongeza Viongozi na Wanachama wote kwa kazi hii kubwa.” Amesema Komredi Kinana

Komredi Kinana, amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (Mbunge wa Bukombe) kwa kubuni na kuleta mawazo hayo ya ujenzi ambayo yalienda Kamati ya Siasa na Halmashauri Kuu na baadaye Wanachama na hivyo uamuzi wa kujenga majengo hayo ulifanyika.

Kutokana na ujenzi wa majengo ya CCM, Bukombe kumfurahisha Komredi Kinana, ameitaka CCM, Mkoa wa Dar es Salaam kujenga Ofisi za kisasa za CCM katika Wilaya zake kama ilivyo Bukombe.

Amesema kuwa, WanaCCM nchi nzima wana wajibu wa kuhakikisha kuwa, Ofisi wanazojenga na kumbi zinafanana na heshima na hadhi ya ukubwa wa CCM kama ambavyo Bukombe walivyotoa heshima hiyo kwa Chama cha Mapinduzi.

Aidha, Komredi Kinana amepongeza umoja na mshikamano ulioko wilayani Bukombe pamoja na Mkoa wa Geita kwa ujumla na kueleza kuwa wao ni Walimu wazuri wa Kusema na Kutenda hivyo atawatuma viongozi wa Chama wa Mikoa na Wilaya kutoka maeneo mbalimbali nchini, waende Bukombe kujifunza mfano wa kuimarisha Chama Kitaasisi na kujitegemea.

Katika hatua, nyingine, Dkt. Kinana ameendelea kuwahamasisha wananchi kujitokeza na kushiriki katika kutoa mchango wao katika mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendelo ya mwaka 2025-2050 ili kuwezesha masuala mbalimbali ikiwemo kufahamu mahitaji ya watanzania na kuweka vipaumbele katika kushughulika na maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemshukuru Makamu Mwenyekiti wa CCM (TZ) Bara, Komredi Abdulrahman Kinana kwa heshima aliyowapa CCM Bukombe ya kuzindua Majengo ya Ofisi.

Ameshukuru Wadau mbalimbali waliochangia katika ujenzi wa majengo hayo wakiwemo WanaCCM wenyewe ndani ya Wilaya ya Bukombe hasa Vijana wa CCM walioshiriki shughuli za ujenzi kwa kujitolea, wananchi wa makundi mbalimbali, baadhi ya Wabunge na viongozi wa Serikali.

Amesema kuwa, mradi unaofuata utahusisha makazi ya Watumishi wa CCM, wakiwemo Makatibu wa Chama ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Ametoa wito kwa Wananchi kuwa na umoja na kueleza kuwa nchi haiwezi kufanikiwa kama watu watachukua muda mwingi kuangalia na kujadili madhaifu ya mtu na kuacha kuangalia mazuri ya mtu kwani suala hili linachelewesha maendeleo ya nchi.

Dkt. Biteko amewataka wanaCCM kuendelea kukiimarisha Chama katika ngazi za chini kwenye mashina na matawi kwani ndiko wananchi wengi walipo.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Mkumba ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Majengo ya CCM yaliyozinduliwa, alisema kuwa, ujenzi huo ni awamu ya Pili ambao unahusisha Ofisi ya CCM na samani zake, Ujenzi wa mgahawa na samani zake ambapo fedha zilizotumika ni shilingi milioni 240, 997,000 ambazo ni fedha za ndani ya Chama Bukombe na ulikamilika tarehe 10 Desemba 2023.

Amesema kuwa mradi huo una faida mbalimbali ikiwemo kuwezesha watumishi kuwa na Ofisi nzuri na vitendea kazi vya kisasa na kupata mapato kupitia mgahawa.

Awamu ya kwanza ya ujenzi wa majengo ya CCM wilayani Bukombe ulihusisha nyumba ya kupumzikia wageni (rest house), yenye hadhi kubwa kitaifa na ukumbi.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa, Mkuu wa Wilaya Bukombe, Said Mkumba, Wakuu wa Wilaya Mkoa wa Geita, Wabunge katika Mkoa wa Geita, baadhi ya Wabunge wa Mkoa wa Kagera na Shinyanga, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Geita, Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Geita na Wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa wa Geita.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages