Na Mwandishi Wetu, Hanang
KAMPUNI ya Mafuta ya Puma Energy Tanzania Limited imekabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea Katesh-Hanang Desemba 3 mwaka 2023 na kusababisha vifo, majeruhi na kuharibu makazi.
Msaada huo wa Puma ni Mifuko 600 ya cement, Mabati 800 na Nondo 1000, vyote vikiwa na gharama na gharama ya Sh.milioni 70 na umepokelewa leo Desemba 28, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja kwa niaba ya Serikali.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania, Bi Fatma Mohemed Abdallah, Meneja Mahusiano wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania Limited Godluck Shirima amesema “ Bodi ya wakurugenzi chini ya Mwenyekiti wake Dk. Selemani Majige, Menejimenti ya Kampuni chini ya uongozi wa Bi Fatma Mohamed Abdallah, wafanyakazi nawameguswa na kuhuzunishwa na mafuriko yaliowakuta wana Katesh.
"Hivyo wakatuelekeza kuleta msaada huu wa vifaa vya ujenzi ili kuunga mkono juhudi na jitiada za Serikali kuwajengea makazi waathirika waliopoteza makazi yao kwenye mafuriko.
"Puma Energy pia ni Muathirika wa mafuriko haya, ambapo kituo chao cha Kateshi kiliharibiwa vibaya na mafuriko, kwa hiyo kama mhanga na mkazi wa Kateshi, kampuni iliona ni vyema kutoa mchango wake kwa jamii ya Katesh, " amesema Shirima.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Hanang Janeth Mayanja ameshukuru msaada huo kutoka kampuni ya Puma Energy amesema, “ msaada huu wa vifaa vya ujenzi kutoka Puma Energy umekuja muda muafaka kwakuwa Serikali sasa ipo kwenye mkakaati wa kuanza kuwajengea wananchi waliopoteza makazi yao kwenye mafuriko.
Amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi makini wa Dk. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuwajengea nyumba wananchi walio poteza makazi na sasa wapo katika hatua za kupima viwanja.
Pia amewaomba wadau wengine kuiga mfano wa Puma Energy na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwasaidia waathirika wa mafuriko na hasa kwa kutoa vifaa vya ujenzi kwa kua ndio vinavyo hitajika zaidi kwa sasa.
Kampuni ya Puma Energy iliwakilishwa na Bw. Godluck Shirima (Meneja Mahusiano), Bi. Lilian Kanora ( Meneja Masoko) na Bw. Joseph Jaruma ( Meneja Rasilimali Watu).
Mkuu wa Wilaya ya Hanang mkoani Manyara Janeth Mayanja (wa pili kulia )akipokea mfuko wa saruji ukiwa ni sehemu ya mifuko 600 ya saruji kutoka kwa Mwakilishi wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania ambaye ni Meneja Uhusiano Godluck Shirima( wa tatu kushoto) Meneja Masoko Lilian Kanora(wa kwanza kulia) na Meneja Rasilimali Watu Bw. Joseph Jaruma ( wa pili kushoto).Wa kwanza kulia ni Ofisa Ugavi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang mkoani Manyara Methew Giramisi .
Mkuu wa Wilaya ya Hanang mkoani Manyara Janeth Mayanja (wa tatu kushoto) akipokea bati kutoka kwa Mwakilishi wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania ambaye ni Meneja Uhusiano Godluck Shirima( wa pili kulia).Wanaoshuhudia Meneja Masoko Lilian Kanora(wa pili kushoto) na Meneja Rasilimali Watu Bw. Joseph Jaruma ( wa kwanza kulia).Wa kwanza kushoto ni Ofisa Ugavi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang mkoani Manyara Methew Giramisi .