Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam ( DAWASA) imeungana na Mamilioni ya watu duniani koye kuadhimisha siku ya Ukimwi Duniani inayoazimishwa kila Desemba moja ya kila Mwaka.
DAWASA imeadhimisha siku ya Ukimwi Duniani kwa kutoa elimu juu ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi, namna bora za kujikinga pamoja na mienendo sahihi ya kuishi baada ya kugundulika kuwa na maambukizi.
Akiongea wakati wa maadhimisho hayo, Mhandisi Jolyce Mwanjee Meneja wa usimamizi wa Mabwawa ya majitaka amesema DAWASA inatambua umuhimu wa kutoa elimu juu ya maambukizi ya Ukimwi kwa watumishi wake ili kuongeza uelewa pamoja na kujua namna sahihi ya kujikinga dhidi ya maambukizi.
"Tuitumie siku hii kujitathimini mienendo yetu ya maisha katika mahala pa kazi na majumbani, niwakumbushe tu kuwa Ukimwi bado upo hivyo tujikinge". amesema.
Mhandisi Mwanjee ametoa wito kwa watumishi wa DAWASA kuzingatia mazoezi, kula vyakula vyenye virutubisho pamoja na kufanya vipimo vya afya mara kwa mara.
"Tujenge utaratibu wa kupima mara kwa mara ili kutambua afya zetu pia tukawe mabalozi wazuri kwa wenzetu bila kunyanyapaa watu wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI" amemaliza
Inakadiriwa kuwa Watu takribani 630,000 hufariki kila mwaka kutokana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
DAWASA inaungana na shirika la Afya Duniani kuwakumbusha wananchi kujilinda dhidi ya Ukimwi.