Breaking

Monday, 11 December 2023

CHINA YAMWAGA VIFAA VYA MAABARA YA UTAFITI WA UVUVI KWA TAFIRI

Naibu katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Daniel Mushi, amepokea ugeni kutoka Jamhuri ya Watu wa China ulioongozwa na Makamu wa Rais wa Chuo cha Sayansi cha China (Chinese Academy of Science – CAS), Prof. Wang Keqiang, katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Wizara zilizopo TEMEKE Veterinari, Jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu alipokea taarifa ya msaada wa vifaa vya maabara vyenye thamani ya dora za kimarekani 190,000 (Tsh. 575,950,000) kutoka kwa Prof. Zhang Ganlin, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Jiografia na Limnolojia ya Nanjing (Nanjing Institute of Geography and Limnology, Chinese Acadeny of Science – NIGLAS). ambaye ameongozana na Makamu wa Rais wa CAS.

Akipokea taarifa hiyo Disemba 7, 2023 kabla ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa kuimarisha ushirikiano katika ulinzi wa mazingira na usimamizi wa rasilimali zilizomo kwenye maji; makubaliano ambayo yanatengeneza fursa nyingine ya kuendeleza utafiti na sayansi.

Prof. Mushi alisema kuwa CAS na NIGLAS wanashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) katika kuendeleza utafiti wa Uvuvi, na wamefanya miradi ya pamoja 5 ambapo wametoa machapisho 9 ya kimataifa ambayo yametuongezea muonekano kama TAFIRI na kama Tanzania, kufundisha wanafunzi 9 wa shahada ya Uzamili na shahada ya uzamivu, kuwezesha maabara ya utafiti za TAFIRI kwa ajili ya kufanya utafiti wa viumbe maji na uvuvi katika Ziwa Tanganyika, na ukanda wa Bahari ya Hindi.

“Kutokana na maendeleo ya kisayansi na Technolojia ambayo China wameyafikia hadi sasa, sisi kama Tanzania tunaona tunafaidika sana kushirikiana na Taasisi mojawapo ya utafiti ya China, na leo Makamu wa Rais wa Taasisi kubwa kabisa ya China CAS (Chuo cha Sayansi cha China) ambayo inasimamia Taasisi zingine zaidi ya 160 za kiutafiti pale China amekuwepo pamoja na sisi na ametuhakikishia kwamba wataendelea kutoa rasilimali nyingi kwa Nanjing Institue of Geography and Technology ili waweze kuendeleza ushirikiano wao na TAFIRI.”

“Sisi kama Nchi tunamuona China kama rafiki wa kweli hata Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa ‘tunao marafiki wengi lakini China ni rafiki wa kweli na hauhitaji kuwa mkomunisti ili ujue kwamba China ana mambo mengi ya kutufunza kuhusu maendelelo’.

Kwa hiyo, kama Nchi na kwa niaba ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunawashukuru sana wenzetu wa China kwa ushirikiano wao wa kweli na kwa kutushika mkono ili kutunyanyua tuweze kufikia hatua ya maendeleo ambayo wao wameweza kufikia.” Alisema Prof. Mushi

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chuo cha Sayansi cha China (Chinese Academy of Science – CAS) Prof. Wang Keqiang alisema kwamba, wapo tayari kushirikiana na Tanzania katika kukuza uchumi wa Buluu, hasa kuongeza nguvu katika tasnia ya ukuzaji viumbe maji katika maji chumvi, upande wa Bahari.

Ameeleza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Sayansi na Teknologia ya China kupitia NIGLAS na TAFIRI una zaidi ya miaka 15, na ulijikita zaidi kwenye maziwa makuu na majibaridi mengine nchini.

Aidha, alisema pamoja na kuwa makubaliano katika ya Wizara ya Sayansi na Teknolojia ya China na Wizara ya Mifugo na Uvuvi yanatoa nafasi ya kukuza sekta ya uvuvi nchini, wataweka mkazo zaidi kwenye tasnia ya ufugaji viumbe maji wa baharini kutokana na msisitizo aliouonyesha Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega (Mb), Waziri wa Mifugo na Uvuvi alipokutana nao katika Uwanja wa Ndege ya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.

Prof. Wang aliongeza kuwa kwa sasa wana taasisi zaidi ya 124 zenye ubobezi tofauti tofauti katika sayansi na teknolojia; kwenye Taasisi hizo kuna watumishi zaidi ya 70,000 wa kada mbalimbali na watumishi zaidi ya 800 wanaounda “think tank” ya China kwenye masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimirei, alisema kwamba Taasisi ya Jiografia na Limnolojia ya Nanjing China na TAFIRI wamekuwa wakishirikiana kwa muda mrefu na wametekeleza miradi mingi ya pamoja inayojumuisha kuwezesha maabara kupata vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufanya utafiti.

Ameongeza kuwa ujio ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofanyika Mwezi Julai mwaka huu kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi paomja na Wizara ya Sayansi na Teknologia ya China ili kuendeleza mashirikiano.

Dkt. Kimirei aliongeza kuwa ugeni huu unanafasi kubwa katika kuendeleza utafiti kwa ujumla, maana Taasisi hiyo ndio “think tank” yaani ni mshauri mkuu wa Serikali ya China kwenye mambo yote yanayohusu sayansi na teknolojia. Disemba 9, 2023 watakwenda Kigoma ambapo Taasisi hiyo imewezesha vifaa vya utafiti kwenye maabara ya TAFIRI ili kuona maendeleo yake, na kuona jinsi ya kupanua wigo wa mashirikiano.
Picha ya pamoja Naibu katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Daniel Mushi (wa tano kutoka kushoto), Makamu wa Rais wa Chuo cha Sayansi cha China (Chinese Academy of Science – CAS), Prof. Wang Keqiang (wa tano kutoka kulia), viongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na baadhi ya wageni kutoka Jamhuri ya Watu wa China mara baada ya kumaliza kikao cha utoaji wa taarifa ya msaada wa vifaa vya maabara vyenye thamani ya dora za kimarekani 190,000 (Tsh. 575,950,000) na utiaji saini mkataba wa kuimarisha ushirikiano katika ulinzi wa mazingira na usimamizi wa rasilimali zilizomo kwenye maji Disemba 7, 2023 kwenye Ofisi za Wizara zilizopo TEMEKE Veterinari, Jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Daniel Mushi akimsikiliza Makamu wa Rais wa Chuo cha Sayansi cha China (Chinese Academy of Science – CAS), Prof. Wang Keqiang (hayupo pichani) katika kikao cha utoaji wa taarifa ya msaada wa vifaa vya maabara vyenye thamani ya dora za kimarekani 190,000 (Tsh. 575,950,000) na utiaji saini mkataba wa kuimarisha ushirikiano katika ulinzi wa mazingira na usimamizi wa rasilimali zilizomo kwenye maji Disemba 7, 2023 kwenye Ofisi za Wizara zilizopo TEMEKE Veterinari, Jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Chuo cha Sayansi cha China (Chinese Academy of Science – CAS), Prof. Wang Keqiang akimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Daniel Mushi (hayupo pichani) alipokuwa akitoa salamu za Wizara katika kikao cha utoaji wa taarifa ya msaada wa vifaa vya maabara vyenye thamani ya dora za kimarekani 190,000 (Tsh. 575,950,000) na utiaji saini mkataba wa kuimarisha ushirikiano katika ulinzi wa mazingira na usimamizi wa rasilimali zilizomo kwenye maji Disemba 7, 2023 kwenye Ofisi za Wizara zilizopo TEMEKE Veterinari, Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimirei akitoa neon la shukrani kwa Naibu Katibu Mkuu Prof. Daniel Mushi na ugeni kutoka Jamhuri ya Watu wa China ulioongozwa na Makamu wa Rais wa Chuo cha Sayansi cha China (Chinese Academy of Science – CAS), Prof. Wang Keqiang, katika kikao cha utoaji wa taarifa ya msaada wa vifaa vya maabara vyenye thamani ya dora za kimarekani 190,000 (Tsh. 575,950,000) na utiaji saini mkataba wa kuimarisha ushirikiano katika ulinzi wa mazingira na usimamizi wa rasilimali zilizomo kwenye maji Disemba 7, 2023 kwenye Ofisi za Wizara zilizopo TEMEKE Veterinari, Jijini Dar es Salaam.
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Daniel Mushi (kushoto), Makamu wa Rais wa Chuo cha Sayansi cha China (Chinese Academy of Science – CAS), Prof. Wang Keqiang (wa tatu kutoka kushoto), viongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na baadhi ya wageni kutoka Jamhuri ya Watu wa China wakibadilishana mawazo mara baada ya kumaliza kikao cha utoaji wa taarifa ya msaada wa vifaa vya maabara vyenye thamani ya dora za kimarekani 190,000 (Tsh. 575,950,000) na utiaji saini mkataba wa kuimarisha ushirikiano katika ulinzi wa mazingira na usimamizi wa rasilimali zilizomo kwenye maji Disemba 7, 2023 kwenye Ofisi za Wizara zilizopo TEMEKE Veterinari, Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimirei (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Jiografia na Limnolojia ya Nanjing (Nanjing Institute of Geography and Limnology, Chinese Acadeny of Science – NIGLAS) Prof. Zhang Ganlin (kulia) wakitia saini mkataba wa kuimarisha ushirikiano katika ulinzi wa mazingira na usimamizi wa rasilimali zilizomo kwenye maji katika kikao cha utoaji wa taarifa ya msaada wa vifaa vya maabara vyenye thamani ya dora za kimarekani 190,000 (Tsh. 575,950,000) Disemba 7, 2023 kwenye Ofisi za Wizara zilizopo TEMEKE Veterinari, Jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia utiaji wa saini hizo ni Naibu katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Daniel Mushi (kushoto) na Makamu wa Rais wa Chuo cha Sayansi cha China (Chinese Academy of Science – CAS), Prof. Wang Keqiang (kulia).
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages