Breaking

Monday, 18 December 2023

BASHE: KUNA FURSA ZA KUTOSHA SEKTA YA KILIMO WAFANYABIASHARA CHANGAMKENI

 

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe

Na Nyabaganga Taraba

Wizara ya Kilimo imekutana na wadau wa Biashara katika Sekta ya Kilimo kwenye Mkutano wa Wawekezaji wa Ndani uliopewa jina la "empowering our own" yaani kujijengea uwezo sisi wenyewe kama Watanzania kwa kuhamasisha wafanyabiashara wa Sekta ya Kilimo waliopo hapa nchini, na wale ambao wanataka kuingia katika uwekezaji katika sekta ya Kilimo.


Mkutano huo umefanyika Serena Hoteli Jijini Dar-es-salaam.


Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema mwelekeo wa Sekta ya Kilimo ni kujilisha wenyewe kama nchi na kulisha wengine. “Our vision is to feed ourself and feed others commercially”. Na kama ndivyo ilivyo, ili kubadilika kutoka kwenye mazoea ya kusema Tanzania inafaa kwa Kilimo tu inabidi tubadilike na tuonane.

“Kama tunataka mabadiliko ya Kilimo tunatakiwa kuonana vizuri tuondoke kwenye msemo wa Tanzania is potential, is potential, is potential tuje kwenye reality”, amesema Bashe.

Waziri wa Kilimo amesema wafanyabiashara wengi wanaofika wizarani kuongelea sekta ya kilimo ni wageni na hilo ndilo limemfanya awaite ili kuwaeleza fursa zilizoko katika sekta hiyo.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukiongea kuhusu uwekezaji wa kutoka nje lakini ushirikishwaji wa wafanyabiashara wa ndani uko wapi”? ameuliza Bashe.
Mhe. Rais amefanya jitihada kubwa kuwekeza katika sekta hii je nini ambacho kinabaki hapa nchini endapo wawekezaji wa nje wanaleta fedha zao na kuwekeza na kutumia hiyo fursa nini kinabaki hapa nchini! nini tunapata baada ya uwekezaji! Amehoji Waziri wa Kilimo.

Ili kuwa na uzalishaji endelevu yatupasa kuzalisha ndani na kuuza duniani, lakini takwimu zinaonyesha kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa chakula barani Afrika na kuwepo ongezeko kubwa la watu wanaokadiliwa kufikia Bilioni mbili (2 billion) ifikapo mwaka 2050. Pamoja na haya, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoagiza chakula kutoka nje ya nchi.
"Lengo letu kama wizara ni kujitosheleza kwa chakula na malighafi na kuuza ziada ya mazao kwaajili ya ukuaji wa uchumi wa nchi. Lakini kwa uhalisia kuna mazao na bidhaa zitokanazo na kilimo ambazo bado tunaagiza kutoka nchi zingine kama ngano, matunda , nyama, bidhaa za maziwa na mboga mboga, mafuta ya kula; ni jambo la kushukuru Mungu kuwa ni kwa upande wa Sukari tumepiga hatua kama sio elinino ya mwaka huu, uagizaji wa Sukari ungekuwa zero(0) lakini miaka mitatu ijayo tutafikia lengo na tutaanza kuuza nje bidhaa hiyo. Uwekezaji katika uzalishaji wa sukari umefanywa na wawekezaji wa ndani kwa sehemu kubwa, amesema Bashe.

Katika wasilisho alilotoa ameeleza kuwa bado kuna uhitaji wa chakula barani Afrika. Lakini wakulima wetu kwa sasa asilimia 82% ni wakulima wadogo wenye wastani wa kulima ekari 2.5 na asilimia 18% iliyobaki ni wakulima wanaolima mashamba makubwa yenye ekari 50-100.

Wataalamu wanashauri kuwa, ili sekta ya kilimo iweze kuwa na mchango zaidi kwa pato la Taifa ni lazima wananchi wanaojihusisha na sekta ya Kilimo wapungue na sekta zingine za utoaji huduma na biashara wawe wengi zaidi.

Ili kufikia hapo, lazima tufanye maamuzi kibiashara kwa kuwawezesha hawa wakulima wadogo kwa kuweka mifumo mizuri ya kibiashara. Kama ni hivyo lazima uwezeshaji ufanyike kwa wakulima hawa wadogo ili watoke kwenye kilimo cha kujikimu na walime kibiashara.

Kuanzia mwaka 1970 – 2020 ukuaji wa sekta ya kilimo umekuwa ukibadilika badilika. kutokana na mabadiliko yaliyokuwa yakijitokeza ya kisera na kiuchumi, kwa sasa tunahitaji kuwa na ukuaji endelevu. Mwaka 2023 tulitakiwa tukue kwa asilimia 7.1 (7.1%), Ili kutekeleza hili tuna hitaji mitaji na uwekezaji.

Na hili lazima lifanywe na Serikali kwa kuweka mifumo mizuri ili biashara ifanyike katika sekta hii, hili litaondoa pia matatizo mengine ambayo yanasababishwa na hali ya maisha ya uzalishaji mdogo unaoleta umasikini.

Lengo kuu la serikali ni kuongeza uzalishaji na tija, wanawake na vijana watawezeshwa kwani kwa taarifa zilizopo makundi haya ni muhimu katika uzalishaji katika sekta ya kilimo.

Waziri Bashe amewakaribisha wafanyabiashara kuwekeza kwenye sekta ya kilimo ambayo ina fursa lukuki ikiwa ni pamoja na maeneo ya uongezaji wa mnyororo wa thamani wa mazao, uzalishaji kwenye mashamba makubwa na utoaji wa huduma zinazohusiana na sekta ya kilimo.

Nae Waziri wa uwekezaji na mipango, Mhe. Prof Kitila Mkumbo (Mb) ameongeza msisitizo katika eneo la uongezaji thamani mazao upewe kipaumbele na uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ufanyike hapa nchini.

Nae Waziri wa fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amesema tutakapozalisha kibiashara tutapunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje. Hivyo kupunguza matumizi ya fedha za kigeni ambazo tunazitumia kuagiza bidhaa za kilimo toka nje ya nchi. Tukiongeza mauzo ya mazao nje ya nchi upatikanaji wa fedha za kigeni hapa nchini itaongezeka lakini pia tutakata mnyororo wa umaskini na tutamiliki uchumi jambo ambalo ni maono ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages