Breaking

Sunday, 12 November 2023

WIZARA ZA NISHATI TANZANIA BARA, ZANZIBAR ZATIA SAINI HATI YA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO





Wizara ya Nishati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Maji, Nishati na Madini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar leo zimesaini hati ya makubaliano itakayopelekea kuimarisha zaidi ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uandaaji wa sera na sheria, utafiti kuhusu uendelezaji wa sekta ya nishati, kubadilishana takwimu, uzoefu, pamoja na utaalam katika maeneo yanayohusu Sekta.

Hati hiyo ya Makubaliano imetiwa saini na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa upande wa Tanzania Bara na Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Mhe.Shaib Hassan Kaduara katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 12 Novemba, 2023.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, kutiwa saini kwa hati hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambao mara kadhaa wametoa maelekezo kwa Wizara hizo mbili kuwa na ushirikiano ili kuendeleza Sekta ya Nishati nchini.

“Viongozi wetu wakisema, kinachotakiwa kutokea ni matokeo ya kile kilichosemwa, vinginevyo tutakuwa hatuwasaidii kama wanasema na hakuna mabadiliko, ninataka niwahakikishie kwamba sisi tunathamini sana mashirikiano tuliyonayo na ushirikiano huu utakuwa endelevu.” Amesema Dkt. Biteko

Ameeleza kuwa, makubaliano hayo yatahusisha Taasisi zilizo chini ya Wizara hizo mbili ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA) , Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).

“Tumesaini hati hizi si kwa ajili ya kupiga picha bali tunataka tuone matokeo yanatokea, hivyo tukafanye ufuatiliaji wa yale tuliyokubaliana, hivyo inabidi tuwe na timu ndogo za kufuatilia yale tuliyokubaliana ili mwisho wa mwaka tupime tumefika wapi. Kwa upande wa Tanzania Bara tutahakikisha kila tulichokubaliana kinatekelezwa.” Amesema Dkt. Biteko

Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko amesema kuwa, msisitizo kwa wananchi wa kutumia nishati safi ya kupikia sasa hautaishia Tanzania Bara pekee bali hatua za uhamasishaji zitafanyika hadi Zanzibar hivyo Wazanzibar watafaidika pia kwa kupata mitungi ya gesi lengo likiwa ni kuwahamasisha kutumia nishati safi ya kupikia.

Kuhusu umeme amesema kuwa, laini ya kV 132 inayotoa umeme Tanzania Bara kwenda Zanzibar imeshazidiwa kwani matumizi ya umeme yameshakuwa makubwa kutokana na shughuli za utalii, viwanda na matumizi mengine hivyo kwa sasa mpango uliopo ni kujenga laini ya kV 220 ili kupeleka umeme wa uhakika Zanzibar.

Akizungumzia makali ya umeme nchini, Dkt.Biteko amesema kuwa, makali ya umeme yanaendelea kupungua kwani kulikuwa kuna upungufu wa megawati 810 lakini sasa umepungua na kufikia megawati 240 na imani iliyopo ni kuwa mwanzoni mwa mwaka 2024 makali ya umeme yatakuwa yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Mhe.Shaib Hassan Kaduara amesema kuwa, hati zilizosainiwa ni nyenzo za kuendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali kwenye Sekta ya Nishati.

Amesema kuwa, wanategemea Wataalam wa Tanzania Bara na Zanzibar wataendelea kushirikiana kwenye masuala mbalimbali ikiwemo la kutatua changamoto ya upotevu wa umeme unaotokana na wizia au masuala mengine ya kitaalam hivyo anaamini wataalam wakishirikiana wanaweza kutatua changamoto hiyo.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ni Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar, Mhe.Shaaban Ali Othman, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Tanzania Bara, Mhandisi Felchesmi Mramba, Katibu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Joseph Kilangi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Zanzibar, Bi.Mwanajuma Abdullah na Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Nishati, Tanzania Bara, Petro Lyatuu.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages