wadau walioshiriki mjadala wa pamoja kati ya Serikali , asasi za kiraia na sekta binafsi juu ya mpango wa Wilaya ya Magu kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi wakiendelea na mjadala wa vikundi wakati wa mjadala huo uliofanyika Novemba 13-15 2023 , katika ukumbi wa mikutano wa Maperece
Mkurugenzi wa shirika la Governence Links Bw. Donald Kasongi akitoa mada wakati wa mjadala wa pamoja kati ya Serikali, Asasi za kiraia na sekta binafsi juu ya mpango wa Wilaya ya Magu kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi unaofanyika katika ukumbi wa Maperece Novemba 14-15 , 2023.
Mratibu wa mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi Wilayani Magu ( MADECC) Bw. Kelvin Makene akizungumza wakati wa mjadala wa pamoja kati ya Serikali, Asasi za kiraia na sekta binafsi juu ya mpango wa Wilaya ya Magu kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi unaofanyika katika ukumbi wa Maperece Novemba 14-15, 2023
Na Mwandishi wetu
Halmashauri ya Wilaya ya Magu inaendelea kutekeleza mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi katika Wilaya hiyo ikiwemo kutekeleza mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi unaotekelezwa katika kijiji cha N'ghaya , kuhamasisha ufugaji wa kisasa, kutoa elimu ya kilimo kinachohimili mabadilikoya tabia ya nchi ili kuunga mkono juhudi za serikali kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Hayo yamebainishwa na Afisa maliasili na mazingira Wilaya ya Magu, Ngussa Buyamba wakati wa mjadala wa pamoja kati ya Serikali , asasi za kiraia na sekta binafsi juu ya mpango wa Wilaya ya Magu kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Maperece ambapo wadau mbalimbali wa mazingira walihudhuria mjadala huo kwaajili ya kujadili mipango mbalimbali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Bw. Ngussa amesema kuwa miradi hiyo inalenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabia ya nchi kwa jamii pamoja na kuijengea uwezo jamii inayoishi katika Wilaya hiyo kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Amesema jamii inajengewa uwezo wa kutumia teknolojia za uvunaji wa maji ya mvua, maji ya chini ya ardhi , kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabia ya nchi , mbinu zinazozingatia mifumo ya ikolojia katika shughuli zao za kijamii na uchumi.
Ameongeza kuwa shguhuli nyingine zinazotekelezwa kupitia mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi Wilayani Magu ni pamoja na kuongeza kipato cha wananchi kupitia kilimo cha kisasa cha bustani na mbogamboga (kupitia vitalu nyumba) vikundi vya ufugaji wa kuku, kondoo, unenepeshajiwa n'gombe, ushonaji nguo na ufugaji wa nyuki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la Governance Link , Donald Kasongi amesema kuwa wameanza mpango wa miaka minne kuanzia Januari 2024, hadi Desemba 2027 wa kusaidia wakulima wadogo kujenga mfumo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi katika sekta ya kilimo.
Amesema shirika hilo linashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Magu na wadau mbalimbali wa maendeleo kuangalia namna ya kuweka mipango ya pamoja na kutafuta rasilimali kwaajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
" Lengo la mjada huu ni kuongeza ushirikiano , kutambua na kuainisha na kuangalia namna ambavyo serikali itahuisha mipango kata iliyoandaliwa katika kata tano ili iingizwe katika mpango wa maendeleo wa Halmashaur" amesema.
Naye mratibu wa mradi wa kukabiliana na mabadiligo ya tabia ya nchi Wilaya ya Magu ( MADECC) , Kelvin Makene amesema programu hiyo imesaidia kuwajengea uwezo vijana kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na kuwezesha vikundi mbalimbali Wilayani humo katika kukabiliana na athari hizo.