Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameonyesha kuvutiwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa na benki ya Exim Tanzania katika kujitanua na kusogeza huduma zake karibu zaidi kwa wananchi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Hatua hiyo ameitaja kuwa itasaidia kukuza uchumi wa maeneo husika na kuimarisha utangamano wa kijamii.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa pongezi hizo jana alipotembelea banda la maonesho la Benki ya Exim Tanzania muda mfupi kabla ya kufungua Maadhimisho ya Wiki ya Huduma ya Fedha yanayoendelea kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Benki ya Exim ni moja ya wadau muhimu wa Maonesho hayo yanayotarajiwa kuhitimishwa Novemba 26, mwaka huu.
Akiwa kwenye banda la benki ya Exim, Waziri Mkuu alipata wasaa wa kupata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo kutoka kwa Meneja Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Bi Kauthar D’Souza ambae pamoja na kuelezea baadhi ya huduma za kifedha zinazotolewa na benki ya Exim Tanzania pia alielezea kuhusu mkakati wa benki hiyo katika kujitanua katika maeneo mbalimbali nchini.
“Niwapongeze sana kwa jitihada mnazoendelea kuzifanya katika kupanua zaidi huduma zenu, hata hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili hizi huduma nzuri mnazoendelea kuzitoa ziwafikie wananchi wengi zaidi hususani waliopo pembezoni huko ambao bado hawajafikiwa na huduma rasmi za kifedha.’’ Alishauri Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa watoa huduma za kifedha nchini kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu ya fedha kwa umma sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji wa huduma hizo zikiwemo riba na ada ili wananchi wengi watumie huduma za fedha zilizo rasmi.
Awali akielezea kuhusu huduma za benki ya Exim Tanzania mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa, Bi Kauthar alisema licha ya jitihada za benki hiyo katika kujitanua zaidi nchini ambapo hadi sasa ina mtandao wa matawi 33 na mawakala 1500 nchi nzima, bado mkakati wake ni kuwekeza zaidi katika utoaji wa huduma kupitia ubunifu wa kidijitali ili kutoa masuluhisho ya kibenki yanayofaa na salama kwa wateja wake.
“Pia tunatambua wajibu tulionao katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi hapa nchini na ndio sababu moja ya kipaumbele chetu ni kuwawezesha watu binafsi na wafanyabiashara wakiwemo wanawake na wajasiriamali kupitia huduma zetu mahususi kwa ajili yao ikiwemo akauti ya Wajasiriamali pamoja na akaunti ya ‘Supa woman’ iliyobuniwa kwa ajili ya wanawake wanaopambana kukuza mitaji ya biashara zao," aliongeza.
Zaidi, Bi Kauthar alibainisha kuwa benki ya Exim Tanzania imeendelea kujitolea kuinua jamii huku akiutaja mpango wa Exim Cares wa benki hiyo kama nguzo muhimu katika utekelezaji wa juhudi mbalimbali za benki hiyo katika kuchangia maendeleo ya nchi kupitia programu zake za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) hususani katika sekta muhimu zikiwemo elimu, afya, michezo na utunzaji wa mazingira (Exim Go Green Initiative).
Katika kuthibitisha dhamira hiyo benki ya Exim kupitia maonesho hayo imeambatana na baadhi ya wajasiriamali wanawake ambao ni wanufaika na Programu ya Uwezeshaji Wanawake (WEP) ya benki hiyo waliopata fursa ya kuonesha bidhaa zao wakiwa kwenye banda la maonesho la benki hiyo lililopo kwenye Maadhimisho hayo.
“Kwa kufanya hivyo, sio tu kwamba tunatimiza wajibu wetu kama benki lakini tumekuwa mawakala wa mabadiliko chanya ndani ya jamii zetu,” alisisitiza.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa pili Kulia) akizungumza na baadhi ya maofisa wa benki ya Exim Tanzania akiwemo Meneja Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Bi Kauthar D’Souza (katikati) na Meneja wa Benki hiyo tawi la Mt.Meru, Arusha Bw Eliud Massaga (wa tatu kushoto) pamoja na mofisa wengine wa benki hiyo wakati alipotembelea banda la maonesho la benki ya Exim muda mfupi kabla ya kufungua Maadhimisho ya Wiki ya Huduma ya Fedha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana. Kulia ni Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa pili Kulia) akizungumza na baadhi ya maofisa wa benki ya Exim Tanzania akiwemo Meneja Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Bi Kauthar D’Souza (wa pili kushoto) na Meneja wa Benki hiyo tawi la Mt.Meru, Arusha Bw Eliud Massaga (kushoto) wakati alipotembelea banda la maonesho la benki ya Exim muda mfupi kabla ya kufungua Maadhimisho ya Wiki ya Huduma ya Fedha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana.
Meneja wa Benki ya Exim tawi la Mt.Meru, Arusha Bw Eliud Massaga (kushoto) akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba (katikati) alipotembelea banda la maonesho la benki hiyo lililopo kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Huduma ya Fedha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana. Kulia ni Meneja Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Bi Kauthar D’Souza
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba (kushoto) akitazama baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wanawake ambao ni wanufaika na Programu ya Uwezeshaji Wanawake (WEP) ya Benki ya Exim wakati alipotembelea banda la maonesho la benki hiyo lililopo kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Huduma ya Fedha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana. Wanaoshuhudia ni pamoja na Meneja Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Bi Kauthar D’Souza (wanne kulia) na Meneja wa Benki hiyo tawi la Mt.Meru, Arusha Bw Eliud Massaga (wa tano kulia)
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba (wa pili kushoto) akizungumza na baadhi ya wajasiriamali wanawake ambao ni wanufaika na Programu ya Uwezeshaji Wanawake (WEP) ya Benki ya Exim wakati alipotembelea banda la maonesho la benki hiyo lililopo kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Huduma ya Fedha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana..
Baadhi ya wajasiriamali wanawake ambao ni wanufaika na Programu ya Uwezeshaji Wanawake (WEP) ya Benki ya Exim akiwemo Bi Rahma Juma (Kushoto), Mariam Mohamed (katikati) na Bi Rahel Nombo wakiwa tayari kuwahudumia wateja wao kwenye banda la maonesho la benki hiyo lililopo kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Huduma ya Fedha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana.