Breaking

Saturday, 11 November 2023

TUGHE YAWAOMBA WAAJIRI KUWEKA PROGRAMU MBALIMBALI KATIKA MAENEO YA KAZI ZITAKAZOSAIDIA KUIMARISHA AFYA ZA WAFANYAKAZI

11 Novemba 2023, Kibaha Pwani

—————————————————

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimewaomba Waajiri kuweka programu mbalimbali katika maeneo ya kazi zitakazosaidia kuboresha Afya za Wafanyakazi na kuleta tija sehemu za kazi.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Cde. Hery Mkunda alipoongoza ujumbe wa TUGHE kushiriki katika Coast City Marathon Iliyofanyika leo Jumamosi, tarehe 11 Novemba 2023, Mkoani Pwani ambapo pamoja naye aliambatana na Mwenyekiti wa Kamati za Wanawake TUGHE Taifa, Ndg. Catherine Katele pamoja na Watumishi na Wanachama wa TUGHE.

Cde. Mkunda ameeleza kuwa TUGHE inatambua umuhimu wa programu hizo katika sehemu za kama vile michezo pamoja na kufanya mazoezi ya mwili kwani huimarisha afya za wafanyakazi na kuwakinga na hatari ya kupata magonjwa hasa yale yasiyo ya kuambukiza sambamba na kuepusha changamoto za Afya ya Akili ambapo yasipodhibitiwa yanaweza kuleta athari kubwa ikiwemo kushuka kwa uzalishaji katika maeneo ya kazi.

Sambamba na wito huo pia Cde. Mkunda amewataka wafanyakazi kushirikiana kikamilifu na Vyama vya Wafanyakazi katika maeneo ya kazi ikiwewamo kujiunga na Vyama hivyo kikiwemo TUGHE ili kuleta umoja miongoni mwao na pia kuboresha afya zao.

Mgeni Rasmi katika Marathoni hii iliyolenga kuchangia ujenzi wa Wodi ya Wazazi katika Hospital ya Rufaa ya Tumbi, alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Aboubakar Kunenge aliyemwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (MB) ambaye amewaomba wadau kuendelea kushirikiana na Serikali kuunga mkono juhudi za Kuboresha Sekta ya Afya nchini.

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimekua kikishirikiana mara kwa mara na wadau mbalimbali kuboresha Sekta ya Afya nchini ikiwemo kutoa misaada ya vifaa katika hospitali kwa kuzingatia kuwa wanachama wa TUGHE pia wanatoka katika Sekta hiyo ya Afya pamoja na Serikali.

Imetolewa na Idara ya habari & Uhusiano -TUGHE

HUDUMA BORA, MASLAHI ZAIDI
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages