Breaking

Thursday, 16 November 2023

TUCTA YAIPONGEZA SERIKALI YA TANZANIA KWA KUSAINI MIKATABA NA SERIKALI YA SAUDI ARABIA ITAKAYOBORESHA AJIRA ZA WATANZANIA NCHINI

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusaini mikataba miwili na Serikali ya Saudi Arabia kwa ajili ya kufungua fursa za Ajira za Watanzania nchini Saudi Arabia.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Cde. Hery Mkunda na kueleza kuwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania limefurahishwa na Uamuzi huo wa Serikali wa kuridhia kusaini Mikataba hiyo na Serikali ya Saudi Arabia kwani itasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha maslahi ya Wafanyakazi, ikiwemo kulinda haki zao na stahiki zao.

Aidha Mikataba hiyo inalenga kuweka mfumo wa kudhibiti mchakato wa kuajiri Wafanyakazi wa kitaalamu na wa majumbani, mifumo ya kisheria, mifumo ya kulinda maslahi na haki za Wafayanyakazi na Waajiri na mifumo rasmi ya kupokea maombi ya ajira, sambamba na kutatua changamoto walizokua wanakutana nazo Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nchini humo.

Aidha kamati ya Pamoja ya wataalamu wa serikali ya Tanzania na Saudia Arabia itaundwa ili kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya ajira, kushughulikia vikwazo na matatizo yatakayojitokeza na kuunganisha juhudi za kusuluhisha panapotokea migogoro kati ya waajiri na waajiriwa. TUCTA inasisitiza ushirikishwaji wa Vyama Vya Wafanyakazi katika kamati hizo kwa ajili ya uwakilishi wa Wafanyakazi.

Sambamba na Pongezi hizo kwa Serikali, TUCTA pia imewakumbusha Wafanyakazi Nchini umuhimu wa kujiunga na Vyama Vya Wafanyakazi ili kuweza kuwa na Sauti Kubwa ya Pamoja katika kushugulikia masuala mbalimbali yanayowahusu Wafanyakazi ikiwemo kupatikana kwa stahiki zao.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages