Breaking

Wednesday, 29 November 2023

TET YASAINI MAKUBALIANO YA UBORESHAJI ELIMU NCHINI

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) leo tarehe 29/11/2023 imesaini makubaliano na taasisi tano zisizo za kiserikali yenye lengo la kuboresha elimu nchini katika nyanja mbalimbali.

Taasisi hizo ni pamoja na Project Zawadi ambao wameingia makubaliano ya kutoa mafunzo kwa walimu na wanafunzi kwa kutoa nyezo bora za mafunzo, Taasisi ya OCODE yenyewe itahusika na kuwafundisha wanafunzi na walimu stadi za maisha ambazo zitaweza kuwasaidia katika maisha ya kila siku.

Taasisi nyingine ni Jenga Hub yenyewe imeingia makubaliano ya kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya teknolojia kwa walimu na wanafunzi, Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope itatoa mafunzo ya lugha ya alama kuanzia ngazi ya Awali hadi vyuo vya ualimu.

Taasisi nyingine ni Right To Play ambayo itaweka maudhui ya miongozo mbalimbali ya mbinu za kusoma kwa njia ya michezo kidigitali (digitization of teaching and learning materials).

Akizungumza mara baada ya kuweka saini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt. Aneth Komba amesema kuwa, Taasisi ya Elimu Tanzania inathamini mchango wa wadau unaoendelea kutolewa katika kuboresha elimu nchini huku akisisitiza TET itaendelea kutoa ushirikiano katika masuala mbalimbali katika eneo la elimu.

“Ninashukuru sana namna ambavyo mmeamua kushirikiana pamoja na sisi, ni suala ambalo Rais wa Jamuhuri ya Muungano ya wa Tanzania analisisitiza katika kuweka ushirikiano na wadau mbalimbali katika kutekeleza majukumu ya Serikali kwa namna ya kuhakikisha wanafunzi nchini wanapata elimu iliyo bora”. Amesema Dkt. Komba.

Ameongeza kwa kusema kuwa makubaliano haya yamekuja wakati muafaka ambapo kumefanyika maboresho ya Sera na Mitaala ya Elimu nchini ambapo kupitia wadau waliongia makubaliano katika kuhakikisha maboresho yaliyofanyika yanatekelezwa.

Kwa upande wa Taasisi hizo zilizoingia makubaliano na TET zimeishukuru Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania kwa kuweka mazingira mazuri ya ushirikiano unaotoa nafasi kwa Taasisi zisizo za Serikali kufanya kazi kwa ubora katika kuwahudumia wananchi hasa katika eneo la Elimu.

Taasisi hizo ni pamoja na Organization for Community Development iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mkuu Bw. Joseph Jackson, Fondation for Disabailities Hope iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mkuu Bw. Maiko Salali, Right To Play iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mkazi, Bi.Maria Mongi, Taasisi ya Jenga Hub iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mkuu, Bi Nancy Sumary, Project Zawadi iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mkuu, Bw. Brian Singer.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages