TANZANIA imesafirisha bidhaa nchini Indonesia zenye thamani ya Sh. Bilioni 64.7 mwaka 2022 huku Indonesia ikiagiza bidhaa nchini Tanzania zenye thamani ya sh. Bilioni 173.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Peter Shelukindo wakati akizungumza katika usiku wa mapokezi na utamaduni yaliyoenda sambamba na maadhimisho ya miaka 78 ya Uhuru wa Indonesia.
Balozi Shelukindo amesema wanapongeza pia uwekezaji wa Indonesia nchini Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo pamoja na gesi asilia huko Mtwara.
Amesema Tanzania wanaweza kupata masoko ya biashara kupitia uwekezaji wa nchi mbalimbali ikiwemo Indonesia na kuahidi kuendeleza uhusiano huo uliodumu kwa takribani miaka 60.
Hata hivyo amesema maadhimisho hayo ya miaka 78 ya uhuru wa Indonesia ni ishara ya urafiki, ushirikiano, maadili ya pamoja ya kitamaduni na kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ya zamani yalianzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1964.
Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo, Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Tri Yogo Jatmiko anasema wanatarajia kuwekeza katika sekta ya nishati na madini hapa nchini.
Aidha anasema Indonesia na Tanzania zimekuwa zikitembea bega kwa bega ili kukuza maendeleo ya vijana na uwezeshaji, kwa kutambua uwezo mkubwa ambao kundi hilo unalo.
"Tunajivunia kusherehekea Siku ya Kitaifa ya Indonesia kwa kuangazia ushirikiano wetu na Tanzania katika uwezeshaji wa vijana. Juhudi zetu za pamoja na Tanzania Bora Initiative zinasisitiza umuhimu wa kulea na kuwawezesha vijana wetu kuwa viongozi, waleta mabadiliko na watu wa muhimj katika jamii zao na kwingineko."
Naye Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Bora Initiative (TBI), Abella Bateyunga aliongeza, “Tunashukuru kushirikiana na Ubalozi wa Indonesia nchini Tanzania. Kupitia huu ushirikiano, tulipata kutumbuiza mbele ya mabalozi 50 na waheshimiwa. Tunamshukuru Balozi wa Indonesia fursa hii muhimu.”amesema