Na Munir Shemweta, WANMM
Serikali imewataka wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya sekta ya ardhi katika kipindi hiki cha maandalizi ya bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa yale maeneo yasiyotengewa fedha za mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi nchini.
Hayo yamebainishwa tarehe 28 Novemba 2023 na Waziri Mkuu Mhe. Kasim Majaliwa katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Wadau Kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika jijini Dodoma.
Kupitia hotuba yake hiyo, Mhe. Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote nchini zinazotekeleza mradi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa timu zinazotekela mradi katika maeneo yao.
‘’Ili mradi ufanikiwe ni vyema wadau wakashiriki kikamilifu katika mradi na nieendelee kuhimiza wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri kutoa ushirikiano kwa timu za utekelezaji mradi’’ alisema Majaliwa
Aidha, amezitaka Taasisi zinazofanya kazi na mradi kama vile NIDA, NEMC, Tume ya Matumizi ya Mipango Bora ya Ardhi na taasisi zote kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi.
Amewataka wataalamu wa sekta ya ardhi kuhakikisha pia wanashirikiana na na viongozi wa serikali za mitaa na vijiji katika kuwapa wananchi elimu kuhusu masuala ya ardhi hususan zile taarifa za utekelezaji mradi.
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amesema, mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi mbali na mambo mengine utajenga ofisi zitakazozingatia mahitaji ya mifumo ya kielektroniki sambamba na kujenga madarasa ya kujifunzia kwenye vyuo vya ardhi vya Morogoro na Tabora.
Kwa mujibu wa Sanga, Wizara ya Ardhi inatumia fursa ya mradi kushughulikia vyanzo vya migogoro ya ardhi pamoja na kuboresha matumizi bora ya ardhi.
‘’Mwaka huu kupitia mradi wa uboreshaji usalama wa milki wizara imepanga pia kurasimisha makazi 500,000 na makazi 100,000 kati ya hayo yatafayiwa kazi na watumishi wa umma na yaliyosalia yakifanyiwa kazi na makampuni binafsi’’ alisema Mhandisi Sanga
Kwa upande wake Waziri wa Madini ambaye ni mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde ameuelezea mradi huo kuwa, utasaidia kuondoa chanagmoto za ardhi pamoja na kuwahakikishia wananchi umiliki wa maeneo yao kwa matumizi mbalimbali na kusisitiza kuwa, mradi huo umekuja wakati muafaka na kubadilisha maisha ya mtanzania.
Januari 2022 Serikali iliingia mkataba wa miaka mitano wa Dola za Kimarekani 150 sawa na Tsh Bilioni 346 na Beki ya Dunia kutekeleza mradi wa uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini, mradi unaojikita kwenye vipengele vya usalama wa milki, mifumo, miundombinu pamoja na usimamizi wa mradi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akizungumza wakati wa Mkutano wa Wadau kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi tarehe 28 Novemba 2023 jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa Wadau kujadili Utekelezaji mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi tarehe 28 Novemba 2023 jijini Dodoma.
Waziri wa Madini ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde akizungumza katika Mkutano wa Wadau kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi tarehe 28 Novemba 2023 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga akizungumza katika Mkutano wa Wadau kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi tarehe 28 Novemba 2023 jijini Dodoma.
Mkuu wa wilaya ya Chamwino mkoa wa Dodoma Gift Msuya akichangia hoja katika Mkutano wa Wadau kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi tarehe 28 Novemba 2023 jijini Dodoma. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)