Breaking

Monday 13 November 2023

KAMATI YA BUNGE YAIPA NGUVU DAWASA KUIMARISHA HUDUMA

Kamati ya Kudumu ya Bunge Uwekezaji na Mitaji ya Umma imeahidi kuendelea kuisaidia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupata fedha za kusambaza huduma ya majisafi kwa wananchi wa maeneo yote ya Dar es Salaam na Pwani.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Deo Sangu (Mb) wakati wa ziara ya kutembelea utekelezaji wa mradi wa maji Chalinze awamu ya tatu unaohusisha upanuzi wa Mtambo wa kuzalisha maji wa Wami.

Amesema kuwa DAWASA inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha huduma ya majisafi inapatikana kwa wananchi wote, kwa kutumia mapato ya makusanyo ya ndani.

Ameongeza kuwa, mojawapo ya maazimio ambayo Kamati imetoa kwa Serikali kwa ajili ya utekelezaji ni pamoja na kuhakikisha madeni ya Taasisi za Serikali zinadaiwa na DAWASA zinalipwa ili kasi ya maboresho ya huduma za maji iendelee kwa kasi ili kuongeza nguvu katika utoaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi wote.

"Pia na madeni ya maji ya taasisi yaweze kulipwa ili kazi ya kusambaza maji kwa wananchi kupitia miradi mikubwa kama huu wa Chalinze awamu ya tatu iweze kuleta tija kwa wananchi, tunaipongeza Menejimenti ya DAWASA kwa jitihada kubwa wanazofanya za kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote." amesema Mwenyekiti Sangu.

"Lengo la ziara ya Kamati hii ni kusimamia utekelezaji wa matumizi ya mitaji ya Serikali kwa taasisi ili tija ya uwekezaji iweze kuonekana." ameeleza.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge ameishukuru Kamati kwa kutembelea na kujionea jitihada zinazofanywa na DAWASA kwa kushirikiana na Mkoa katika kufanikisha adhma ya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama ndoo kichwani.

Amesema kuwa kwa sasa upatikanaji wa majisafi kwenye Mkoa wa Pwani ni asilimia 85, ongezeko linalovutia uwekezaji mkubwa wa viwanda.

Ameiomba Bunge kupitia Kamati kuiwezesha DAWASA kupata fedha zaidi za kusambaza maji kwa wananchi wote wanufaika wa miradi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete ameieleza Kamati juu ya jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali kupitia DAWASA za kutekeleza mradi wa Chalinze awamu ya tatu pamoja na mradi wa maji Mlandizi - Chalinze - Mboga ambao umekamilika na umeleta unafuu.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa mradi wa maji Chalinze ulipitia hatua mbalimbali za utekelezaji kuanzia awamu ya kwanza, ya pili na sasa awamu ya tatu ambayo inaendelea.

Kwa awamu hii ya tatu ambayo imegharimu Bilioni 83, mradi unahusisha upanuzi wa uwezo wa Mtambo wa Wami kutoka uzalishaji wa lita milioni 7.2 kwa siku hadi lita milioni 21.6 kwa siku.

Ameongeza pia kuwa, mradi umehusisha ujenzi wa matenki 18 ya kuhifadhi maji pamoja na ujenzi wa vioski 351 vya kuchotea maji ambavyo tayari vimekamilika.

"Mradi umelaza bomba la usamabazaji maji kwa umbali wa kilomita 826, na unalenga kunufaisha wakazi wa vijiji zaidi ya 56," ameeleza Ndugu Kingu.





Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages