Breaking

Sunday, 19 November 2023

JUMLA YA WALIMU 1832 WA MADARASA YA AWALI WATAKIWA KUWA WATEKELEZAJI WAZURI WA SERA

Jumla ya walimu 1832 wa madarasa ya Awali ambao wameshiriki mafunzo ya Mtaala mpya ambapo wametakiwa kuwa watekelezaji wazuri wa Sera iliyoboreshwa yenye kujumuisha mtaala mpya wa elimu nchini.

Agizo hilo limetolewa leo tarehe 19/11/2023 na Naibu Katibu Mkuu Or-TAMISEMI Dkt.Charles Msonde wakati akifunga mafunzo ya walimu kazini kuhusu mtaala mpya ambapo amesema kuwa,walimu wanapaswa kuwa watekelezaji wazuri ili serikali ifikie malengo ya utoaji elimu iliyo bora.

"Nawapongeza walimu wote nchini kwakweli ninajivunia sana walimu wa kitanzania wa shule za msingi na sekondari katika taifa letu la Tanzania mnafanya kazi nzuri sana na kuwa Sera hii iliyoboreshwa pamoja na mtaala mpya ulioboreshwa ni zao la watanzania kwa sababu ni watanzania ndio wamesema iwe hivi, watanzania na wadau mbalimbali ndio wameshiriki kutoa mawazo yao, na hayo mawazo ndio haya yamewekwa ili tuweze kuyatekeleza vizuri"amesema Dkt.Msonde.

Pia, amesema kuwa serikali kwa makusudi imeamua kuhakikisha kwamba inamaliza kero zote za walimu nchini kwa kutatua changamoto mbalimbali ili kuhakikisha wanafanya kazi yao kwa weledi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt.Aneth Komba ameeleza kuwa kufuatia kukamilika kwa kazi ya uboreshaji wa mitaala ya elimu kuanzia Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu kwa lengo la kuwajenga wahitimu wenye ujuzi utakaowawezesha kujitegemea au kujiajiri pia utakaowawezesha kutumia vyema fursa zinazopatikana nchini kwa kumudu maisha yao ya siku kwa siku kujiajiri au kuajiriwa pale wanapohitimu mafunzo.

Amesema anaamini walimu waliopata mafunzo hayo watakwenda kuwapa ujuzi walimu wengine na kuweza kuwa bora katika ufundishaji wao.

Mafunzo hayo yamefanyika kuanzia tarehe 13 hadi 19 Mwezi Novemba katika mkoa wa Iringa ambapo yanatarajiwa kufanyika katika mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam kwa kuwahusisha walimu wa Elimu ya Awali nchini.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages