Breaking

Monday, 27 November 2023

Hospitali ya Aga Khan kufanya upasuaji 25 kurekebisha maumbile kwa wanawake na wasichana 25 wenye majeraha ya moto

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam imepanga kufanya pasuaji 25 za kurekebisha maumbile kwa wanawake na wasichana 25 wenye majeraha makubwa ya moto, kasoro kubwa za kimwili, na wahanga wa ukatili wa kijinsia ambayo yatafanyika kuanzia Novemba 28 hadi Desemba 02, 2023.

Matibabu hayo yatasimamiwa na timu mahiri ya madaktari wa kimataifa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile kutoka Marekani, Canada, na Ulaya. Watashirikiana kwa karibu na madaktari wa Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaama, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Bugando, na Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 27, 2023 Jijini Dar es Salaam, Daktari Mwandamizi wa Upasuaji, na Mkuu wa Idara ya Upasuaji katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, Dkt. Athar Ali amesema kuwa awali, zaidi ya wanawake na wasichana 60 wenye matatizo yanayohusiana na majeraha ya moto na wanaosumbuliwa na changamoto za ukatili kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania walifanyiwa uchunguzi bila gharama yoyote, ikiwemo chunguzi zilizofanywa Zanzibar.

"Baadaye, wanawake 25 na wasichana 7 walichujwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kubaini ustahiki wao wa kufanyiwa upasuaji. Mwishowe, wanawake na wasichana 25 waliokidhi vigezo stahiki vya upasuaji wa kurekebisha maumbile walichaguliwa kufanyiwa matibabu bila gharama yoyote". Amesema

Aidha amesema kuwa kama sehemu ya mradi huo, madaktari wa kimataifa wa upasuaji watashirikiana kivitendo na wataalamu wa afya wa Tanzania, wakiwaonesha mbinu mbalimbali za upasuaji wa kurekebisha maumbile ili kuimarisha utaalamu mahalia wa upasuaji wa kurekebisha maumbile.

Amesema kuwa Ijumaa ya Desemba 01, 2023, Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam itaendesha semina ya Elimu Endelevu ya Kitiba (CME) kwa zaidi ya wataalamu wa afya 100, ikilenga kukuza uelewa wa suala la upasuaji wa kurekebisha maumbile.

Nae Daktari Bingwa wa Upasuaji na Kiongozi wa Timu ya Reconstructive Women International, Dkt. Andrea Pusic amesema kuwa "huu ni mwaka wa 8 wa ubia wetu madhubuti na Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam na Hospitali ya Taifa Muhimbili. Ushirikiano huu umeleta ongezeko kubwa sana la utaalamu na uwezo wa madaktari mahalia wa upasuaji wa kurekebisha maumbile. Kwa pamoja, tumeweza kuhudumia mamia ya wanawake na wasichana waliojeruhiwa ili kuboresha utendaji wa kimwili na mwonekano wao.”

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji katika Hospitali ya Aga Khan, Dkt. Aidan Njau amesema “Kwa mara nyingine tena Hospitali yetu ya Aga Khan itafanya pasuaji kubwa za kurekebisha maumbile kwa wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania wenye changamoto kubwa kama vile majeraha ya moto, ajali, nk., na kusababisha sehemu za miili yao kuharibika vibaya. Programu hii ya siku 5 itawasaidia hasa wanawake na wasichana, kwa kuwa hili ndiyo kundi linaloathiriwa zaidi na changamoto hizi. Kwa sababu ya wahisani waliojitolea kuendesha programu hii, uchunguzi na matibabu yanatolewa bila gharama yoyote. Programu hii inaendeshwa kila mwaka na madaktari bingwa kutoka Ulaya na Marekani, na kila mwaka tunapata ushirikiano na shauku kubwa kutoka kwa Watanzania. Ningependa kuchukua fursa hii kuwakumbusha Watanzania kutumia vizuri fursa hii ya matibabu, ambayo kwa kawaida ni aghali sana lakini sasa yanapatikana bure.”

Dkt. Edwin Mrema, ambaye ni Mkuu wa Upasuaji wa Kurekebisha Maumbile katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, amesema, “Sisi kama Madaktari wa Upasuaji wa Kurekebisha Maumbile, wasaa wa kuridhisha zaidi katika kazi yetu ni pale tunaposaidia kurejesha tabasamu na hali ya kujiamini iliyopotea kwa wanawake na watoto.”

Bw. Sisawo Konteh, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Aga Khan, amewashukuru wahisani kwa michango yao mikubwa ya kifedha kwa ajili ya kuunga mkono pasuaji hizo kwa miaka mingi. Ametaja baadhi ya mambo waliyojifunza katika miaka iliyopita, ikiwemo kushirikiana na taasisi ya Lady Fatemah Trust kuongeza usaidizi wa afya ya akili kwa wagonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji ili kukidhi mahitaji yao ya kisaikolojia na kuwasaidia kurejea katika maisha yao ya kawaida. Pia ametoa shukrani zake kwa vyombo vya habari kwa kuwaunga mkono katika kipindi cha miaka 8 iliyopita.

Katika kuunga mkono jitihada hii kubwa, ufadhili wa matibabu haya unapatikana kutoka vyanzo mbalimbali kama vile Programu ya Ustawi wa Wagonjwa ya Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam, Reconstructive Women International, Khalid Islamic Foundation, Lady Fatemah Trust, Corporate partners (Stanbic, DTB, Generic, Planet & Centurion ), na watu binafsi wenye nia njema. Michango hii ya kifedha ina jukumu muhimu katika wigo mpana wa matibabu haya, ikijumuisha mahitaji ya kabla ya upasuaji kama vile uchunguzi wa kitiba, hatua ya upasuaji inayojumuisha kufanyiwa upasuaji na kukaa hospitalini, uangalizi baada ya upasuaji unaohusisha usafishaji wa vidonda na urejeshaji wa mwili katika utendaji wa kawaida, na kutoa usaidizi wa chakula na malazi kwa ndugu wa wagonjwa.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages