Breaking

Wednesday, 15 November 2023

DKT. BITEKO AZUIA VIFAA VYA UMEME KUNUNULIWA NJE YA NCHI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa katazo kwa kampuni zinazosimamia na kutekeleza miradi ya umeme nchini, kutonunua nje ya nchi vifaa vya umeme ambavyo vinazalishwa hapa nchini ili kukuza viwanda vya ndani vinavyozalisha vifaa hivyo, kuvipa thamani, kukuza ajira na uchumi wa nchi.

Dkt. Biteko ametoa agizo hilo tarehe 15 Novemba, 2023 mkoani Mtwara wakati alipokagua miradi ya umeme vijijini na kuwasha umeme katika Kata ya Naliendele, eneo la Pachota A na Kijiji cha Nachenjele.

" TANESCO na REA, tabia ya kununua vifaa vya umeme nje ya nchi hiyo ni zilipendwa, viwanda vipo ndani ya nchi halafu vifaa vinanunuliwa nje, hivi vifaa vyetu mnataka tukauze wapi, kuanzia leo na kuanzia nilivyoingia ndani ya ofisi lazima bidhaa zinazozalishwa hapa zinunuliwe na vifaa visivyopatikana ndani ya nchi ndio viagizwe kutoka nje, tukuze viwanda vyetu, tuvipe thamani na kukuza ajira." Amesema Dkt. Biteko

Aidha, Dkt. Biteko amewataka wakandarasi wa umeme vijijini kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kueleza kuwa Serikali itafanya tathmini ya kila mkandarasi kuona alivyotekeleza miradi na ambao hawafanyi vizuri watasitishiwa mikataba kwani Serikali inalipa wakandarasi hao na itaendelea kuwalipa hivyo hawana sababu za kukwamisha Miradi ya Upelekaji Umeme Vijijini.

"Angalieni mabilioni yaliyomwagwa kwenye Mkoa wa Mtwara, shilingi bilioni 170 zimeletwa hapa kusambaza umeme vijijini ambazo zitafaidisha pia maeneo ya mijini lakini yanafanana na kijijini, lengo letu ni mwezi wa sita mwakani kumaliza kazi ya kupeleka umeme vijijini na kuhamia vitongojini." Amesema Dkt. Biteko

Pamoja na kuwapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kusimamia vyema kazi ya kusambaza umeme, amewataka kutokucheka na wakandarasi hao ili kazi ya kupeleka mahitaji ya umeme kwa wananchi ifanyike kwa ufanisi.

Katika katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaeleza wananchi wa Mtwara juhudi mbalimbali zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwapelekea maendeleo kama vile ujenzi wa miundombinu ya kielimu, afya, barabara na upanuzi wa bandari ya Mtwara ambao utapelekea usafirishaji wa korosho kufanyika kwa urahisi, mafuta kushushiwa katika bandari hiyo na makaa ya mawe kusafirishwa kutokea Bandari ya Mtwara.

Kutokana na hilo, Dkt. Biteko amewataka Watendaji wa Serikali kusimamia ipasavyo fedha za Serikali na amemuagiza Mkuu wa Mkoa Mtwara kuwachukulia hatua wale wote wanaorudisha nyuma hatua za maendeleo.

Vilevile, Dkt. Biteko amewaasa wananchi kuungana katika kujiletea maendeleo bila kuangalia itikadi za vyama kama ambavyo Serikali inapeleka miradi ya maendeleo kwenye maeneo yote.

Akiwa katika Kijiji cha Nachenjele, Dkt. Biteko ameagiza Shule ya msingi na sekondari katika Kijiji hicho kupelekewa umeme na pia ametoa Kompyuta tano kwa shule ya sekondari na tano kwa shule ya msingi.

Awali, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Jones Olotu alimweleza Naibu Waziri Mkuu kuwa, Mkoa wa Mtwara umetengewa shilingi bilioni 170 kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini na kwamba katika vijiji 785 vya mkoa huo, Vijiji 401 bado havina umeme lakini wakandarasi kampuni ya Derm, Central na Namis wanaendelea kusambaza umeme kwenye Vijiji vilivyosalia.

Ametaja miradi inayoendelea kutekelezwa mkoani humo kuwa ni REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili (REA III Round II), Mradi wa kusambaza umeme katika maeneo ya pembezoni mwa miji (Vijiji-Miji) (Peri-Urban III), Mradi wa Kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo, Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji pamoja na Mradi wa ujazilizi (Densification 2C).



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages