Breaking

Saturday 18 November 2023

DAWASA YATAKIWA KUTOA HUDUMA YA MAJI KWA MALIPO KIDOGOKIDOGO

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha kila wananchi anawezeshwa kupata huduma ya majisafi kwa kupewa utaratibu wa kulipa kidogokidogo kwa mkopo.

Ametoa kauli hiyo kwenye hafla ya utiaji saini na kumkabidhi mkandarasi M/S SINOHYDRO kutoka China eneo la utekelezaji wa mradi wa Majk Bangulo.

Amesema kuwa sio wananchi wote wanakuwa na uwezo wa kulipia gharama ya maunganisho mapya kwa wakati kulingana na utofauti wa kipato, hivyo kwa wale ambao hawawezi wapewe utaratibu wa kulipa kwa njia ya mkopo ili wote wanufaike na huduma ya majisafi.

"Kwa sasa upatikanaji wa maji kwenye maeneo mengi ya Jiji la Dar es salaam huduma umeimarika, hivyo ni vyema kila mwananchi apate huduma kikamilifu ili kufanikisha adhma ya Serikali ya kumtua Mama ndoo kichwani." ameeleza Mhe Aweso.

"Tunapaswa kumshukuru Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa aliyoufanya wa fedha za ukamilishwaji wa miradi hii na usambazaji wa majisafi kwa wananchi kwenye maeneo mengi, hivyo tunapaswa kuhakikisha wananchi wanaona tija ya uwekezaji huu kwa wao kupata maji." amesisitiza Mhe. Aweso.

Kuhusu mradi wa maji wa Dar es Salaam ya Kusini maarufu kama mradi wa Bangulo, Mhe. Aweso amesema mradi huo mkubwa utaenda kunufaisha wakazi wapatao 450,000 wa majimbo mbalimbali ya *Ukonga, Segerea, Ubungo, Kibamba, Ilala na Temeke* na kuongeza kuwa mradi huu ni wa muhimu sana kwa kuwa wananchi wa maeneo haya wamekuwa kwenye changamoto ya maji kwa muda mrefu, hivyo kumtaka mkandarasi ahakikishe anatekeleza mradi ndani ya wakati ili ukamilike na wananchi wapate maji.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Segerea , Mhe. Bonna Kamoli ameishukuru Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza nguvu nyingi katika kumtua Mama ndoo kichwani kupitia mradi huu wa maji, hii inaleta matumaini makubwa kwa wananchi ambao wamekuwa kwenye changamoto ya maji kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa utekelezaji wa mradi huu wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji Dar es Salaam ya Kusini utaenda kutatua changamoto ya maji kwenye Jimbo la Ilala, Ubungo, Temeke, Ukonga, Ubungo na sehemu ya Jimbo la Kisarawe.

Ameongeza kuwa mradi kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia kwa bilioni 36.967, na ambao unalenga kunufaisha wananchi 450,000 wa majimbo matano ya uchaguzi.

"Utekelezaji wa mradi umegawanyika katika awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza utanufaisha Kata za Kwembe, Kitunda, Pugu Stesheni, Kipunguni na Mzinga. Awamu ya pili itahudumia wakazi wa Kata kata za Kivule, Kinyerezi, Zingiziwa, Majohe, Charambe, Kwembe, Buza, Msongola, Msigani na Mbezi," ameeleza Ndugu Kingu.

Mradi unahusisha ujenzi wa tenki la kuhifadhi na kusambaza maji lenye ukubwa wa lita milioni 9 litakalojengwa eneo la Bangulo, ujenzi wa bomba la kusafirisha maji la ukubwa wa inchi 28 kwa umbali wa kilomita 10.8 pamoja na bomba la kusambaza maji kwa umbali wa kilomita 17.29.

Pia kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa maji kwenye makazi ya wananchi, Mamlaka imetenga fedha za utekelezaji wa miradi midogo mbalimbali ambapo kwa Jimbo la Kibamba Mamlaka imetenga milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kunufaisha wakazi 12,200 wa maeneo ya mbezi makabe, Kitopeni na maeneo ya jirani.





Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages