Breaking

Friday 10 November 2023

DAWASA YAKABIDHI MADAWATI 30 VIKAWE


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam DAWASA imekabidhi jumla ya Madawati 30 katika shule ya Msingi Vikawe ikiwa kama sehemu ya kutambua na kuchangia Ukuaji wa elimu katika jamii inayoihudumia.

Akizungumza na wazazi pamoja na uongozi wa shule katika hafla fupi ya makabidhiano shuleni hapo, Mgeni rasmi Mkurugenzi wa huduma kwa wateja DAWASA CPA (T) Rithamary Lwabulinda ameahidi ushirikiano zaidi katika shule hiyo ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika Mazingira rafiki.

"DAWASA kupitia utaratibu wake wa kurudisha katika jamii sehemu ya kile wanachokipata tumeweza kusaidia Madawati haya 30 tukitambua uhitaji mkubwa uliopo shuleni hapa ili kuwezesha wanafunzi kusoma katika Mazingira rafiki" ameeleza Lwabulinda

Lwabulinda ameongeza kuwa kwasasa DAWASA ni sehemu ya jamii ya watu wa Vikawe na hivyo wataendelea kuwa bega kwa bega katika utoaji wa huduma na pindi yatokeapo mahitaji kadri ya itakavyofaa.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Vikawe ndugu, Jegama Selemani ameishukuru DAWASA kwa msaada waliowapatia na kuomba isiwe mwisho wa mahusiano mazuri kati ya shule hiyo na Mamlaka.

"Shuleni kwetu hapa tulikua na uhitaji mkubwa wa Madawati, DAWASA wamechangia asilimia 40 ya uhitaji wa Madawati Leo hii, jambo ambalo litawezesha wananfunzi 90 kuondokana na kusoma wakiwa wamekaa chini" ameeleza ndugu Jegama.

Ndugu Maulid Hamduni ameipongeza Mamlaka kwa kazi kubwa inayofanya katika utoaji wa huduma ya Majisafi lakini kwa kuijali jamii inayoihudumia pindi inapokua na uhitaji.

"Msaada huu kwetu kama wazazi ni ahueni kubwa, wengi wetu tuna kipato cha chini na hata tunapojaribu kuchangishana muda mwingine hatufikii malengo, Madawati haya yatasaidia watoto wetu kusoma vizuri na kupata ufaulu wa hali ya juu" ameeleza ndugu Hamduni

Shule ya Msingi Vikawe yenye jumla ya wanafunzi 900 ni Moja ya taasisi nufaika na utaratibu wa DAWASA kurudisha kwa jamii sehemu ya huduma yake Ili kuleta tija kwa wananchi wa eneo lote la kihuduma lililopo chini ya Mamlaka.





Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages