Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kupitia idara ya Usafi wa Mazingira imejidhatiti vyema kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa Mazingira hasa kipindi hiki cha mvua zinazoendelea.
Akizungumza shughuli mbalimbali za usafi wa Mazingira zinazoendelea Mhandisi Mbaraka Mohamed ameeleza kuwa Mamlaka imejipanga vyema kukabiliana na changamoto zozote zinazoweza kusababisha uchafuzi wa Mazingira.
"Kwasasa tunaendelea na maboresho mbalimbali ya chemba za majitaka kote katika Jiji la Dar es salaam, hii inaenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya Majitaka sehemu mbalimbali za Jiji ili kuhakikisha inafanya kazi Kwa ufanisi na uchafuzi wa Mazingira unahepukika" ameeleza Mhandisi Mbaraka.
Mhandisi Mbaraka ameongeza kwa kuwataka wananchi kuwa na matumizi sahihi ya miundombinu ya majitaka kwa kuacha tabia ya kutiririsha majitaka mitaani hasa kipindi hichi cha mvua pamoja na utupaji wa taka ngumu unaopelekea kuziba kwa miundombinu hiyo na kusababisha uchafuzi wa mazingira.
"Tuna timu yenye watu wa kutosha, tumegawanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji ili kuhakikisha huduma inakua bora, mwananchi anapopata changamoto yeyote asisite kutupigia kupitia namba 0735 451879 au kufika katika ofisi za DAWASA zilizo karibu nae na tutamfikia kwa haraka" ameeleza Mhandisi Mbaraka.
Ndugu Irene Moshi, mkazi wa Mikocheni amepongeza juhudi zinazofanywa na DAWASA katika kukabiliana na changamoto ya majitaka mitaani.
"Tatizo la Majitaka kutiririka mitaani lilitusumbua na kutuweka katika hatari ya kupata magonjwa, lakini kazi kubwa inayofanywa na DAWASA usiku na mchana imetupa imani kuwa tupo katika Mazingira salama na afya zetu hazipo Mashakani" ameeleza ndugu Moshi.
Mamlaka inasisitiza matumizi sahihi ya miundombinu ya majitaka kwa wananchi wote ikitambua umuhimu wa afya za wateja inaowahudumia na kutoa kipaumbele katika usafi wa Mazingira.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990