Breaking

Thursday, 16 November 2023

DAWASA YAANZA KUTUMIA MITA ZA LIPA KABLA (PRE - PAID METER)


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea na zoezi la uboreshaji wa mfumo wa mita za maji za kulipia kabla ya matumizi kwenye vioski vya maji katika mji wa Chalinze ili kuongeza ufanisi zaidi wa huduma.

Zoezi la uboreshaji wa mita hizi za kisasa linatekelezwa na wataalam wa ndani wa Mamlaka mara baada ya kukamilika kwa kazi ya kubuni na kusanifu teknolojia hii iliyoasisiwa mapema mwaka wa fedha 2023/2024.

Akizungumza juu ya mapinduzi hayo, Afisa Tehama DAWASA Mhandisi Emmanuel Mwanyamaki amesema kuwa zoezi la kufunga mita za lipa kabla lilianza Septemba mwaka huu na sasa kazi ya maboresho inaendelea ili kuongeza ufanisi zaidi katika kutoa huduma ya maji.

"Mpaka sasa tumefanikiwa kufunga mita hizi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo vituo vya Maji Mdaula, Chamakweza, Pingo na Mwindu, na tunaendelea na maboresho lakini pia tupo katika mchakato wa utekelezaji kwenye maeneo mengine." ameeleza Ndugu Mwanyamaki.

"Kwa eneo la Chalinze, kuna jumla ya vioski vya maji 550, na kwa kuanzia tumefunga kwenye vioski zaidi ya kumi na zoezi litaendelea ili kukamilisha kwenye vioski vyote," amesema Mhandisi Mwanyamaki.

Ameongeza kuwa teknolojia hii ya mita za kulipa kabla ina manufaa mengi kwa wateja ikiwemo kupunguza upotevu wa maji pamoja na kuepusha upotevu wa fedha kwa wasimamizi wa vioski.

Amewaomba wasimamizi wa vituo vya maji Chalinze kuendelea kuwa mabalozi wazuri na waangalizi wazuri wa miundombinu hii ya maji ili idumu na kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwidu, Ndugu Hassan Mtemvu ameishukuru DAWASA kwa kuja na ubunifu mzuri wa mita za lipa kabla kwani italeta nafuu ya changamoto mbalimbali kwenye huduma ya maji.

"Ubunifu huu ni mzuri na utawawezesha wananchi kupata huduma bora na ya uhakika, na pia kupunguza upotevu wa maji mitaani.” ameeleza Mwenyekiti Mtemvu

Kwa upande wake Bi Ester John msimamizi wa kituo cha majo eneo la Mdaula ameeleza kufurahishwa na mfumo huu wa mita za kulipa kabla kwa kuwa inawasaidia kuondokana na madeni ya kwa Mamlaka.

Kuanza kwa matumizi ya mita za maji za kulipia kabla ni sehemu ya mapinduzi makubwa ya teknolojia yaliyotekelezwa na DAWASA na yatakayosaidia katika kupunguza upotevu wa maji mitaani, kupunguza gharama za ufuatiliaji madeni kwa sehemu za mbali.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages