Breaking

Monday, 13 November 2023

CCM NA CPV KUNUFAISHA SEKTA YA UZALISHAJI TANZANIA

 



Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Komredi Daniel Godfrey Chongolo akizungumza na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV), Komredi Prof. Le Hai Binh, leo Jumatatu, Novemba 13, 2023, Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam. Ndugu Prof. Le, na ujumbe aliombatana nao, yuko ziara ya kikazi kwa siku tatu nchini Tanzania.
***

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Godfrey Chongolo amesema kuwa chama hicho kinaridhishwa na urafiki na uhusiano wake na Chama cha Kikomunisti cha Viet Nam (CPV), na kipo tayari kuendeleza ushirikiano kati ya pande hizo mbili utakaoongeza fursa kwa Tanzania kunufaika zaidi, hasa kupitia nyanja za sayansi na teknolojia, kukuza uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, maeneo ambayo Nchi ya Vietnam ina uzoefu mkubwa. 

Katibu Mkuu Chongolo amesema kuwa kupitia mahusiano ya kihistoria yaliyopo kati ya CCM na CPV, kisiasa, kijamii na kiuchumi, vyama hivyo vitaimarisha zaidi misingi itakayotumiwa na Serikali za nchi zote mbili, Tanzania na Vietnam katika kubadilishana uzoefu na mikakati sahihi ya kubadili hali za maisha ya watu, kupitia sekta ya uzalishaji, ambayo ni hatua muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa na kipato cha mtu. 

Komredi Chongolo amesema hayo alipokutana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CPV, Komredi Prof. Le Hai Binh, leo Jumatatu, Novemba 13, 2023, kwenye mazungumzo ya kikazi yaliyofanyika Ofisi Ndogo za Ofisi ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam. 

“Kama ulivyosema Komredi Profesa Le Hai Binh, kuhusu kupandisha hadhi ya urafiki, ushirikiano na uhusiano wetu huu, CCM iko tayari, kama ambavyo ninyi mko tayari. Urafiki wetu huu wa kihistoria ambao umekuwa sawa na undugu, umekuwa ni urafiki wa nyakati zote na majira zote, kisiasa, kiuchumi na kijamii, ukijengwa katika misingi ya itikadi na falsafa za tangu waasisi wa vyama hivi viwili na mataifa haya mawili.”
“Ni muhimu sasa tija yake iende mbali na kuonekana dhahiri katika kusaidia kubadilisha hali za maisha ya wananchi waliotupatia ridhaa na dhamana ya kuongoza. Katika eneo hilo la uzalishaji Vietnam mmepiga hatua kubwa na mna uzoefu mkubwa. Eneo la matumizi ya sayansi na teknolojia pia mmeenda mbali sana. Maana kwa sasa hata kilimo na mnyororo wake sayansi na teknolojia imechukua nafasi kubwa sana ili kuwa na uzalishaji na thamani yenye tija. Sisi Tanzania tunayo mengi ya kujifunza kutoka Vietnam,” amesema Komredi Chongolo na kuongeza;

“Serikali za CCM zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa CCM na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, zimeweka mikakati na msukumo mkubwa na katika eneo la uzalishaji, katika sekta zote, kama kilimo, ili kukuza na kuimarisha uchumi.”

Katibu Mkuu Chongolo alimwambia Komredi Prof. Le Hai Binh kuwa kupitia Mpango wa Kisera wa DOI MOI, Vietnam ilifanikiwa kupiga hatua kubwa ya mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo ya watu wake, akitoa mfano kuwa ndani ya miaka 25 iliyopita uchumi wake umekua kwa kasi, ambapo kwa sasa thamani ya fedha za mazao inayouza nje imefikia Dola za Marekani Bilioni 20, ikitoka kuwa mmoja wa waagizaji wakubwa wa mchele na kahawa, duniani mnamo miaka ya 1990 na sasa inashika nafasi ya pili kwa kuuza mchele nje na nambari tatu kwa kuuza kahawa. 

“Haya ndiyo tunataka tujifunze, tubadilishane uzoefu, mafunzo na hata nyenzo ili Tanzania isongee mbele zaidi.”

Kwa upande wake Komredi Prof. Le Hai Binh, aliye anataka na ujumbe wake, alisema kuwa thamani ya Chama Cha Mapinduzi, Serikali yake na Nchi ya Tanzania kwa ujumla mbele ya CPV na Vietnam, ni kubwa mno, kwa sababu za kihistoria, ambapo vyama hivyo na nchi zote mbili zina mtazamo mmoja wa itikadi ya kisiasa na kiuchumi, na historia imewapitisha katika ushirikiano wa mapambano wa watu wanyonge kujikomboa. 

“Kitu kingine ambacho nchi zetu hizi mbili, chini ya uongozi wa CCM na uongozi wa CPV vinaweza kujivunia na kugeuza kuwa ni fursa kwa kila moja kunufaika, ni kuwa katika maeneo mazuri kijiografia. Nchi ya Tanzania chini ya CCM ni lango la nchi nyingi za Afrika. Hivyo hivyo, kijiografia Vietnam kijiografia iko katika eneo ambalo ni lango kwa nchi nyingi za Asia.

“Hii ni fursa kwa nchi zote mbili kushirikiana. Tuko tayari kupandisha hadhi ya urafiki na ushirikiano wetu kati ya CCM na CPV kwa ajili ya Tanzania na Vietnam ili tusaidiane katika kuongeza uzalishaji, kukuza uchumi na pato la mtu na kuboresha hali za maisha ya watu wetu,” amesema Komredi Prof. Le Hai Binh. 

Ndugu Prof. Le Hai Binh ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Tawala cha Vietnam, CPV, pamoja na ujumbe aliombatana nao watakuwa chini Tanzania kwa ziara ya siku tatu, ambapo watakutana na Uongozi wa Chama na Serikali.

********************************



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages