NA EMMANUEL MBATILO, BAGAMOYO
BODI ya Wakurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetembelea katika bandari ya Bagamoyo na Mbweni kwa lengo la kutazama mambo yanavyofanyika katika ukaguzi wa bidhaa na changamoto zinazopatikana ili kuboresha shughuli za ukaguzi katika bidhaa zinazoingia kupitia bandari hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa habari katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi TBS, Prof. Othman Chande amesema kuwa wamefika mahali hapo na wamegundua changamoto kadhaa mojawapo ikiwa ni jinsi upakuaji mizigo husika unavyofanyika.
"Mafuta yanavyoingia hapa yanatupwa baharini watu wanasukuma kutoa nje hii mbinu siyo nzuri sana , ila kwa sasa inabidi tuende nayo tu hivyohivyo Amesema Prof.Chande.
Naye Kaimu Meneja wa Kanda ya Mashariki Bw.Fransis Mapunda amesema kuwa wanaishukuru Bodi ya wakurugenzi ya TBS kuwatembelea na kuwapa muongozo jinsi ya kutatua changamoto wanazopitia hasa katika kuhakikisha bidhaa zinazoingia nchini zinakidhi matakwa ya viwango.
Amesema katika Bandari hiyo wana ofisi ambayo imekuwa ikikagua mizigo inayoingia na inayopitia hapo kwenda visiwani Zanzibar na sehemu nyingine mbalimbali.
Pamoja na hayo Bw. Mapunda ametoa wito kwa wafanyabiashara kutumia ofisi ya TBS kupitisha mizigo yao kwani ni kituo rasmi kilichowekwa na serikali ili kuepuka hasara itakayopatikana baada ya kukamatwa kwa yule ambaye anakiuka utaratibu uliowekwa.
"Mizigo inayofika katika bandari hii ikichukua muda mrefu, inachukua masaa sita inakua imesha shughulikiwa itoke katika eneo hili hivyo basi natoa wito kwa wafanyabiashara wapitie kupitisha mizigo yao tuweze kuikagua kwa maana wakipitisha sehemu nyingine ile mizigo ikikamatwa itakua hasara kwao kwani itaenda kuteketezwa". Amesema Bw. Mapunda
Kwa Upande wake Mfanyabiashara wa Mafuta Bw.Frank Kimaro ameipongeza TBS kwa kuwapatia huduma nzuri ambayo haina usumbufu kwao kama wafanyabiashara hivyo amewaomba wafanyabiashara ambao wamekuwa wakienda kinyume na utaratibu uliowekwa na TBS kuacha kutumia njia zisizo sahihi na kuweza kupitia TBS ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa wafanyabiashara.