Breaking

Friday, 17 November 2023

BENKI YA NBC YATOA ELIMU YA KIFEDHA KWA WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI TAMBAZA.

Dar es Salaam: Novemba 17, 2023: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa elimu ya masuala ya kibenki na umuhimu wa kujijengea utamaduni wa uwekaji akiba kwa wanafunzi wa Shule ya Shule ya Sekondari Tambaza iliyopo Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo inalenga kutoa fursa kwa wanafunzi hao kujifunza masuala ya kifedha ili kuwajengea utamaduni wa kujiwekea akiba, kubuni mawazo ya biashara sambamba na kutambua namna ya kutumia taasisi za kifedha kukijenga kiuchumi.

Semina fupi kuhusu mafunzo hayo ilifanyika jana shuleni hapo ikiongozwa na Mkuu wa Uendeshaji NBC Bi. Alelio Lowassa alieambatana na viongozi wengine waadamizi wa benki hiyo akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Benki ya NBC,Bi Salama Mussa, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi wa Mahesabu wa benki hiyo Bw Fulgence Shiraji pamoja na maofisa wengine waandamizi. Wenyeji waliongozwa na Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Hussein Mavumba, baadhi ya walimu pamoja na wanafunzi.

Akizungumzia hatua hiyo Bi Lowassa alisema ni muhimu kwa kuwa inalenga kuwajengea ufahamu na ujuzi wa kifedha vijana hao wakiwemo wale wanaotarajia kuhitimu elimu ya sekondari na kujiunga elimu ya juu na wale watakaojiri.

“Elimu ya fedha kwa wanafunzi ni muhimu kwa sababu inawawezesha kuelewa mapema jinsi ya kutunza na kuendesha fedha zao, kubuni na kufuata bajeti, na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha. Pia, inawafundisha umuhimu wa akiba, uwekezaji, na matumizi sahihi ya mikopo. Tunaamini hawa ndio wajasiriamali, wawekezaji na maofisa wa kesho hivyo ni vema kuanza kuwaandaa mapema ili pia waweze kujua namna ya kutumia taasisi za fedha katika kujikwamua. Hatua hii ni mwendelezo tu wa jitihada zetu kwenye elimu ambapo kupitia mpango wetu wa Wajibika tunatoa 'Scholarship' kwa wanafunzi 1000 kwa wanafunzi wa VETA hapa nchini,’’ alibainisha.

Alisema ukosefu wa elimu ya fedha na ujasiriamali miongoni mwa wanafunzi imekuwa ikisababisha baadhi yao wanapohitimu shule kushindwa kwenda sambamba kasi ya uchumi kwenye jamii zao hivyo hujikuta kwenye dimbwi la umaskini hasa pale wanapokosa ajira hatua ambayo imekuwa ikisababisha baadhi yao kuingia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya na vitendo vingine viovu na visivyo na maadili kwa jamii.

Mafunzo hayo yalihusisha uwasilishwaji wa mada mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, ujasiriamali pamoja na kutoa fursa kwa wanafunzi hao kujibu na kujadili hoja mbalimbali kuhusu mada hizo. Zawadi mbalimbali ikiwemo jezi za vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya NBC Premier League, mipira na zawadi binafsi zilikabidhiwa kwa uongozi wa shule pamoja na wanafunzi mbalimbali. Wakiwa shuleni hapo maofisa wa benki hiyo pia walishiriki zoezi la upandaji miti ya matunda na vivuli kwenye viunga vya shule hiyo.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Mavumba pamoja na kuishukuru Benki ya NBC kwa hatua hiyo, alisema elimu hiyo itawasaidia wanafunzi hususani wale wanaotarajia kuhitimu kuwa na elimu ya kujiwekea akiba, kujijjenga kijasiriamali hata pale watakaposhindwa kuendelea na elimu ya juu zaidi.

“Elimu hii ni muhimu sana, ni bahati mbaya tu sio wanafunzi wote wamekuwa wakiipata. Wanafunzi wanaohitimu sio wote wanaofanikiwa kupata ajira bali wapo wengi ambao wanaamua kujiajiri wao wenyewe. Inapotokea hivyo elimu ya ujasiriamali na matumizi sahihi ya fedha inaweza kuwa na msaada zaidi kwao. Hata wale wanaoendelea na elimu ya juu elimu hii huwasaidia sana kujiwekea akiba na kutumia vizuri fedha wanazopewa na serikali kama mikopo ya kujikimu huko vyuoni…tunawashukuru NBC kwa elimu hii na zawadi mbalimbali walizotupatia,’’ alishukuru.

Wakizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzao, wanafunzi Siti Omary na Erick Massawe waaliishukuru Benki ya NBC kwa kutoa mafunzo hayo wakiahidi kuyafanyia kazi hususani kwenye eneo la kujiwekea akiba. Zaidi wanafunzi hao waliahidi kuendelea kuwa mabalozi wa kueneza elimu hiyo kwa wanafunzi wengine kutokana na umuhimu wake.

"Tunaishukuru sana NBC kwa kuamua kuleta elimu hii muhimu kwetu. Tunaamini elimu hii itatolewa pia kwa wenzetu kwenye shule nyingine kwasababu wanafunzi tulio wengi bado tunakabiliwa na changamoto ya kutokujua umuhimu wa akiba na ukosefu elimu ya ujasiriamali. Hii ndio sababu tumeshuhudia wenzetu wengi wamekuwa wakikwama kuendesha shughuli binafsi wanapohitimu na hivyo kutegemea ajira ya kuajiliwa,’’ alisema Mwananfunzi Siti.


Mkuu wa Uendeshaji NBC Bi. Alelio Lowassa (aliesimama) akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tambaza iliyopo Manispaa Ilala jijini Dar es Salaam walioshiriki semina fupi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha na akiba iliyoendeshwa na benki hiyo shuleni hapo jana. Wanaomsikiliza ni pamoja na Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Hussein Mavumba (wa pili kulia), walimu na maofisa wengine waandamizi wa benki hiyo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tambaza iliyopo Manispaa Ilala jijini Dar es Salaam Mwalimu Hussein Mavumba (aliesimama) akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo walioshiriki semina fupi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha na akiba iliyoendeshwa na benki ya NBC shuleni hapo jana. Wanaomsikiliza ni pamoja na maofisa  waandamizi wa benki hiyo akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Benki ya NBC,Bi Salama Mussa (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi wa Mahesabu wa benki hiyo Bw Fulgence Shiraji (wa tatu kushoto)

Mkuu wa Uendeshaji NBC Bi. Alelio Lowassa (kushoto) akikabidhi mpira wa miguu kwa Mwalimu Nicholaus Nolasco ambae ni mwalimu wa Michezo Shule ya Sekondari Tambaza ya jijini Dar es Salaam ikiwa ni moja ya zawadi zilizotolewa na benki hiyo kwa uongozi na wanafunzi wa shule hiyo wakati semina fupi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha na akiba iliyoendeshwa na benki hiyo shuleni hapo jana. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Hussein Mavumba (wa pili kshoto), walimu, wanafunzi na maofisa wengine waandamizi wa benki hiyo.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi wa Mahesabu wa benki ya NBC  Bw Fulgence Shiraji (kushoto) akikabidhi mpira wa miguu kwa mmoja wa wanafunzi  wa Shule ya Sekondari Tambaza ya jijini Dar es Salaam ikiwa ni moja ya zawadi zilizotolewa na benki hiyo kwa uongozi na wanafunzi wa shule hiyo wakati semina fupi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha na akiba iliyoendeshwa na benki ya NBC shuleni hapo jana. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Uendeshaji NBC Bi. Alelio Lowassa (katikati) na Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Hussein Mavumba (wa pili kulia)

Mafunzo hayo yalihusisha uwasilishwaji wa mada mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, ujasiriamali pamoja na kutoa fursa kwa wanafunzi hao kujibu na kujadili hoja mbalimbali kuhusu mada hizo.

Meneja Huduma wa Benki ya NBC Bw. Stanley Munisi akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tambaza iliyopo Manispaa Ilala jijini Dar es Salaam walioshiriki semina fupi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha na akiba iliyoendeshwa na benki hiyo shuleni hapo jana.

NBC Daima! Baada ya semina hiyo viongozi wa Benki ya NBC wakiongozwa na Mkuu wa Uendeshaji NBC Bi. Alelio Lowassa (wa tano kushoto) ulipata wasaa wa kupiga picha ya pamoja na walimu walimu pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tambaza wakiongozwa na Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Hussein Mavumba (katikati).

Mkuu wa Uendeshaji NBC Bi. Alelio Lowassa (Katikati) sambamba na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi wa Mahesabu wa benki hiyo Bw Fulgence Shiraji (kushoto) na Mkuu wa shule ya Sekondari Tambaza Mwalimu Hussein Mavumba (kulia) wakipanda moja ya mti wa matunda kwenye viunga vya shule hiyo ikiwa ni kumbukumbu ya ziara ya maofisa hao shuleni hapo kwa ajili ya semina fupi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha na akiba kwa wanafunzi. Wanaoshuhudia ni maofisa wengine wa benki hiyo.

Baadhi ya maofisa wa benki ya NBC wakipanda moja ya mti wa matunda kwenye viunga vya shule ya Sekondari Tambaza ikiwa ni kumbukumbu ya ziara ya maofisa hao shuleni hapo kwa ajili ya semina fupi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha na akiba kwa wanafunzi. Wanaoshuhudia ni maofisa wengine wa benki hiyo.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages