Breaking

Saturday, 14 October 2023

WAZIRI MKENDA AFUNGA MAFUNZO YA UONGOZI, USIMAMIZI WA SHULE KWA WAKUU WA SHULE ZA MSINGI

Serikali imesema baada ya kukamilika na kupitishwa kwa rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 itaanza kufanya mapitio ya sheria za elimu.

Akizungumza Oktoba 13, 2023 Mjini Bagamoyo wakati wa kufunga mafunzo ya uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shule kwa Wakuu wa Shule za Msingi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema mchakato huo utaanza mara baada ya tamko la kuanza kwa utekelezaji wa sera hiyo.

Kiongozi huyo amefafanua kuwa ili Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 itekelezwe kwa ufanisi, Sheria ya elimu ya Mwaka 1978 na Sheria nyingine zinazohusu elimu ni lazima zifanyiwe mapitio ili kuiwezesha kwenda sambamba na mabadiliko ya elimu yatakayofanyika nchini.

"Rasimu ya sera inayotarajiwa kuanza kutumika mwakani imeweka mkazo katika ubora wa walimu, mkazo katika kuwaendeleza walimu walio kazini na pia tutawachuja wanaoingia katika kada hiyo ili kulinda hadhi walimu, tunataka walimu bora na si bora walimu" amesisitiza Waziri huyo

Prof. Mkenda amesema mabadiliko ya mitaala yamekwenda sambamba na mapitio ya Sera kwa kuwa katika raaimu ya sera kuna mabadiliko makubwa yamefanyika na kwamba rasimu ya mitaala hiyo ipo katika tovuti ya Taasisi ya Elimu Tanzania na kuwataka wadau na wananchi kuisoma na kuielewa.

Amewaambia Wakuu wa Shule hao wanaporudi katika maeneo ya kazi kuwa vinara na chachu ya kuhakikisha mageuzi hayo makubwa ya elimu yanafahamika kwa wadau na wananchi.

Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo Waziri Mkenda amesema Serikali itaendelea kuimarisha mafunzo kwa walimu kazini kwa kupitia Vituo vya Walimu (TRCs) na yatakayokuwa yakifanyika katika Mikoa, kanda na Kitaifa ili kuwajengea umahiri.

Aidha, Prof Mkenda amewataka Wakuu hao wa shule kuhakikisha wanasimamia maadili ya walimu hasa katika suala la malezi na usalama wa watoto wanaowafundisha.

Ameongeza kuwa kwenda kinyume na maadili hayo kunaharibu sifa ya walimu pamoja na kuumiza wanafunzi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongonzi wa Elimu (ADEM) Dkt. Sixtone Masanja amesema mafunzo hayo kwa awamu ya kwanza yanahudisha mikoa saba ambapo jumla ya Walimu Wakuu 4,516 wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea umahiri katika uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shule

Mtendaji Mkuu huyo ameongeza kuwa mafunzo mengine yaliyotolewa ni pamoja na uendesshaji wa ofisi ya Mkuu wa Shule, ukusanyaji wa takwimu na uaandaaji wa mpango wa jumla wa maendeleo ya shule na Motisha kwa walimu.

"Mafunzo haya yameandaliwa baada ya kufanyika kwa utafiti na kusoma tafiti nyingine za wanazuoni wengine juu ya uongozi na usimamizi wa shule na elimu kwa ujumla na tafiti hizo zilionyesha uhitaji wa mafunzo kwenye maeneo hayo , hivyo tuna imani kubwa baada ya mafunzo Wakuu wa Shule wataenda kusimamia shule zao kwa ufanisi zaidi na kuinua ubora wa elimu" amesisitiza Dkt. Masanja.

Naye Mkuu wa Shule ya Msingi Juhudi iliyopo Morogoro Naomba Msuyu Manispaa amesema mafunzo hayo yametolewa kwa wakati unaofaa kwani yatawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hasa kutokana na mageuzi makubwa ya elimu yanayotarajiwa kufanyika
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages